02 July 2012

Mapigano makali yaibuka Tegeta *Msafara wa Rais wanusurika kupigwa mawe


Na Willbroad Mathias

ENEO la Tegeta Namanga, lililopo Manispaa ya Kindondoni, Dar es Salaam, jana liligeuka uwanja wa vita baada ya wakazi wa eneo hilo kupambana vikali na askari wa Kampuni Binafsi ya Ulinzi ya NAS Secority iliyopewa kazi ya kobomoa nyumba za wakazi hao.

Wakati vurugu hizo zikiendelea, msafara wa Rais Jakaya Kikwete uliokuwa ukipita eneo hilo kwenda Bagamoyo, ulinusurika kupigwa mawe na wakazi wa eneo ambao waliweka vizuizi barabarani.

Vurugu hizo zilitokea saa tatu asubuhi, baada ya askari na mabaunsa 97, kufika eneo hilo wakiwa na mmiliki wa Kituo cha Mafuta cha GAPGO na kuanza kubomoa nyumba zipatazo 10 katika eneo hilo.

Wakizungumza na Majira, mashuhuda wa tukio hilo, walisema baada ya askari hao kuanza kubomoa nyumba hizo, wananchi walikuja juu na kuanza kuwafukuza kwa mawe.

Kutokana na hali hiyo, askari hao walilazimika kutumia risasi za moto ili kuwatawanya wananchi ambao hawakuonesha dalili ya kukubali na kuzidi kuwashambulia askari hao kwa mawe.

“Baada ya hawa askari kuona wananchi hawaogopi risasi za moto, waliamua kutimua mbio, wakati vurugu zikiendelea, msafara wa Rais Kikwete ulikuwa ukipita ambapo wananchi waliuzuia kwa kuweka vizuizi barabarani.

“Msafara ulipunguza mwendo ambapo wananchi walikuwa wakirusha mawe kwa mbali ingawa hakuna gari iliyoumia,” alisema shuhuda huyo ambapo tukio hilo limethibitishwa na Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Charles Kenyela.

Mwandishi wetu alipofika eneo la tukio, alishuhudia samani mbalimbali za wakazi wa eneo hilo ambao nyumba zao zimevunjwa zikiwa zimetupwa nje.

Wakizungumza na Majira, baadhi ya waathirika walidai kuishi eneo hilo zaidi ya miaka 50 iliyopita, lakini wanashangaa kuambiwa eneo hilo si mali yao.

“Wakati mmiliki wa kituo hiki cha mafuta anasimamisha jengo katika eneo hili, sisi tayari tulikuwa tumeanza kuishi muda mrefu, hata kilipouzwa kwa mmiliki mwingine ambaye ni kampuni ya Big Born, tulishuhudia kila kitu,” alisema.

Walisema mmiliki wa kituo hicho amevunja sheria kwa sababu kama alitaka kuwaondoa, alipaswa kuwapa taarifa lakini eneo hilo bado lina kesi ya msingi iliyopo katika Mahakamani Ardhi ambayo wananchi wanapinga kubolewa nyumba zao.

“Mimi marehemu baba yangu ndiye alikuwa mtu wa kwanza kuishi eneo hili kabla kituo hiki hakijajengwa,” alisema mkazi wa eneo hilo Bi. Stina Idd.

Akizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, Kamanda Kenyela alisema hadi sasa wanawashikilia watu 97 ambao wanadaiwa kushiriki kubomoa nyumba hizo.

“Miongoni mwa watu tunaowashikilia ni mtu aliyewaleta walinzi wa kampuni hii ambaye ni mmiliki wa Kapuni ya Big Born, askari wa kampuni ya NAS Security na madalali kutoka Kampuni ya Msolopa Auction Mart,” alisema Kamanda Kenyela.

Alisema mbali na kukamatwa watu hao, asakari wawili wa kapuni hiyo walijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Mwananyamala.

No comments:

Post a Comment