02 July 2012
Hali ya Dkt. Ulimboka yabadilika ghafla
Stella Aron na Rehema Maigala
JOPO la madaktari sita wanaomtibu Dkt. Steven Ulimboka, limesema kiongozi huyo wa Jumuiya ya Madaktari nchini, amepata mtikisiko katika ubongo wake ambapo jana limetokea tatizo la kitaalamu wakati wakiendelea kuokoa maisha yake.
Dkt. Ulimboka anaendelea na matibabu katika Chumba wa Wagonjwa Wanaohitaji Uangalizi Maalumu (ICU), kilichopo Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Akizungumza waandishi wa habari, Kiongozi wa jopo la madaktari hao, Profesa Joseph Kihamba, alisema jana mchana hali ya Dkt. Ulimboka ilibadilika ghafla lakini bado anaendelea vizuri.
“Bado tunaendelea kumfanyia uchunguzi wa kina katika mwili wake kutokana na majeraha makubwa aliyoyapata, Dkt. Ulimboka ameumia sehemu mbalimbali na kusababisha apate maumivu makali,” alisema.
Wakati huo huo, Chama cha Wauguzi Tawi la MOI (TANNA), jana limetoa tamko la kuitaka Serikali kutatua haraka mgomo uliopo ambao unachangia kusababisha mzigo mkubwa.
Akizungumza na Majira, Mwenyekiti wa tawi hilo, Bi. Prisca Tarimo, alisema chama hicho kinalaani vikali kitendo cha
kinyama kilichofanywa kwa daktari huyo.
“Tunaiomba Serikali ifanye ifanye uchunguzi wa haraka kuwabaini wote waliohusika kufanya kitendo cha kinyama kwa Dkt. Ulimboka, ili tuondokane na matatizo yanayojitokeza hivi sasa,” alisema.
Aliongeza kuwa, mgomo unaoendelea sasa ni mzigo mkubwa kwa wauguzi ambao wanabebeshwa lawama wasizostahili kuzipata.
Kutokana na mgomo unaoendelea MNH, jana baadhi ya wagonjwa waliokwenda kutafuta matibabu walishindwa kuingia taasisi ya MOI baada ya geti lake kufungwa na kufuli.
Mkazi wa Dodoma, Bi. Lydia Rwechungura, ambaye ni mtumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Wilaya ya Chamwino, alifika hospitalini hapo lakini alikosa huduma.
“Nimefika hapa kwa ajili ya kupata huduma ya mgongo maana kila ninapotembea pingili zinajisaga na kupata maumivu makali lakini nasikitika kuambiwa huduma zozote sijui nifanyeje,” alisema.
Hata hivyo, Bi. Rwechungura alidai kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Dodoma kwenda MOI.
Jana asubuhi waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali walikusanyika MOI lakini uongozi wa taasisi hiyo ulifunga geti bila kutoa sababu za kufanya hivyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment