Na Waandishi Wetu Tumaini Maduhu na Masau Bwire
RAIS wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Bw. Gratian Mukoba, amesema chama hicho hakijali vitisho na propaganda zitakazotolewa na wajiri wao (serikali), na wananchi kutokana na mgomo uliopangwa kuanza Jumatatu asubuhi.
Akizungumza na waandishi wa habari Daresalaam jana, Bw. Mukoba alisema mgomo huo umezingatia taratibu na sheria za utumishi wa umma ambapo suala la vitisho ni jambo la kawaida.
Alisema propaganda zilizotolewa hadi sasa ni pamoja na tamko Serikali likiwataka walimu wapuuzie mgomo huo kwa madai ni batili kutokana na shauri lao kuwa mahakamani.
“Sisi kama CWT tunasema kuwa, mgomo upo pale pale, hatuogopi vitisho vyovyote kwa sababu wanachama wenyewe ndio wameafiki kwa asilimia 95.7 ambao ni walimu wa shusle za awali, msingi, sekondari, maofisa walioko kwenye ukaguzi wa shule pamoja na wakufunzi wa Vyuo na Ualimu na Maendeleo ya Jamii,” alisema.
Bw. Mukoba aliwataka walimu kushiriki mgomo huo akidai ni halali na umeitishwa na CWT kwa mujibu wa sheria na hauna uhusiano wowote na ushiriki wao katika sensa ya watu na makazi.
Hata hivyo, alisema walimu wanapaswa kutambua kuwa madai kuwa shauri lao lipo mahakamani, hakiwaondolei utararatibu wa kuendelea na mgomo kwani hadi sasa, mahakama haijatoa amri yoyote ya kusitisha mgomo huo.
“Kutokana na hoja hiyo, tunaisishi Serikali isitake kutumia kivuli cha mahakama kugandamiza haki za walimu ambao wamezingatia taratibu na sheria zote za nchi kufanikisha mgomo.
“CWT tunatoa wito kwa walimu wote nchini, kuunganisha nguvu zao ili tupate haki zetu tunazoidai Serikali bila kujali vitisho ambavyo vinaendelea kutolewa,” alisema Bw. Muhoba.
Wakatu huo huo, Mwandishi Wetu kutoka Ruvuma anaripoti kuwa, CWT mkoani humo, kimesisitiza kuwa, suala la mgomo lipo pale pale kama ulivyopangwa.
Msisitizo huo umetokana na ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms), uliotumwa na Bw. Mukoba kwa viongozi wa chama hicho ukiwataka wanachama wa CWT kutoenda kazini Jumatatu.
Walisisitiza chombo kinachotakiwa kutoa tamko la kusitisha mgomo huo ni mahakama pekee si wapinzani wao ambao ni Serikali.
Katika Mkoa huo, walimu asilimia 97 wameunga mkono mgomo uliotangazwa na CWT ambapo kundi dogo la walimu hao ndilo halijapiga kura ya kuunga mkono.
Taarifa kutoka ndani ya chama hicho mkoani hapa zinasema kuwa, pamoja na Serikali kuwa na utamaduni wa kukimbilia mahakama, kifungu cha 84/ (1) (e) cha sheria ya ajira na mahusiano kazini ya mwaka 2004, kinairuhusu Mahakama ya Kazi kuweka zuio baada ya kujiridhisha wahusika wameshiriki katika mgomo batili.
Kifungu cha 84/(2) kinaizuia mahakama kutoa amri hiyo hadi zipite saa 48 baada ya maombi ya zuio kufikishwa kwa aliyeitisha mgomo ambaye ni CWT.
Mwenyekiti wa CWT, mkoani hapa, Bw. Castory Ngonyani na Katibu wa chama hicho Bw. Luya Ngonyani, waliwataka walimu kusikiliza kauli za chama na sio ya Serikali.
Katika hatua nyingine, wakati CWT kikitangaza mgomo huo nchi nzima kuanzia Jumatatu, baadhi ya walimu wamegawanyika hasa mkoani Dar es Salaam na Pwani, wakidai hawako tayari kugoma bali wataingia kazini na kuchapa kazi kama kawaida.
Wakizungumza na Majira jana kwa sharti la kutotajwa majina yao gazetini, baadhi ya walimu wa shule mbalimbali, walisema mgomo uliotangazwa na CWT kupitia Rais wake Bw. Mukoba, hauna manufaa kwao bali unalenga masilahi yake na viongozi wa kitaifa.
Walidai viongozi CWT ngazi ya Taifa, wamewageuza walimu kuwa mradi wao kwa kutangaza migomo ya msimu ili upande wa pili uwaone, kuwapoza chochote na kutangaza mgomo hakuna.
“Kimsingi tumechoshwa na mchezo wanaotufanyia, kama ni suala la kugoma, agome yeye na kamati yake, mwaka 2008 Bw. Mukoba alitangaza mgomo lakini siku moja kabla haujaanza, tulikusanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, akatangaza mgomo hakuna.
“Katika mkutano ule kulikuwa na wawakilishi kutoka mikoani tukiamini tunatangaziwa taratibu za kufanya ili kufanikisha mgomo, alivyotangaza mgomo hakuna tulikasirika na kumpiga kwa chupa za maji kwani tulijua tayari amehongwa,” walisema na kuongeza kuwa, hivi sasa hawauungi mkono kwani wamechoka kudanganywa.
Walisema ndani ya uongozi wa CWT wenyewe hawaelewani kwa sababu ya fedha wanazokatwa walimu ambapo hadi sasa, mgogoro huo umeshindwa kutatuliwa.
“Walimu wote nchini tunakatwa kila mwezi asilimia mbili ya mshahara wetu, hatujawahi kuambiwa fedha hizi zinatumika vipi, hatuoni faida yoyote zaidi ya viongozi CWT kula fedha zetu.
“Kama CWT haitutendei haki, moyo wa huruma wameutoa wapi hadi kuishinikiza Serikali ipandishe mshahara kwa asilimia 100 kama si kutaka kujikosha kwetu, hatugomi hadi tuambiwe fedha zinazokatwa zinatumika vipi vinginevyo tutawafikisha mahakamani kwa ufisadi wanaotufanyia,” walisema walimu hao.
Alisema hivi sasa, walimu wanajipanga ili kuandaa maandamano makubwa ya kupinga uongozi wa CWT kwani chama hicho mbali ya kuchukua ada ya uanachama, kimeshindwa kugharamia sare za walimu hasa wanapoadhimisha siku yao kitaifa.
“Kila siku tuaambiwa chama hakina fedha wakati michango yetu kwa mwezi mmoja inatosha kununua fulana kwa walimu wote, wao wana fedha zetu wanashindwa kutuhudumia iweje waishutumu Serikali hadi kuitisha mgomo, kwanza watutendee haki kabla ya kuomba nguvu yetu,” walisema.
Majira lilipomtafuta Bw. Mukoba ili kuzungumzia madai hayo, alimwambia mwandishi wetu amtafute baada ya saa mbili kwani yupo kwenye kikao na muda huo ulipofika, simu yake ya mkononi ilikuwa haipatikani.
Waandishi wa haabari hii ni Tumaini Maduhu, Masau Bwire na Steven Augustino.
No comments:
Post a Comment