30 July 2012

Saintfiet aanza tambo Jangwani *Apania kuivua ubingwa Simba


Na Speciroza Joseph

BAADA ya kutwaa Kombe la Kagame kwa mara ya kwanza, Kocha wa Yanga, Tom Saintfiet amewapongeza wachezaji wake na kutamba huo ni mwanzo bado Ligi Kuu Bara na mashindano mengine.

Yanga juzi ilitwaa kombe lake la tano la Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup) ikiwa chini ya kocha huyo aliyeanza kuifundisha timu hiyo wiki tatu zilizopita akichukua mikoba ya Kostadin Papic aliyetimuliwa.

Mabingwa hao walitwaa kombe hilo mara ya pili mfululizo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya kulipa kisasi kwa kuichapa Azam FC 2-0 kwenye mchezo wa fainali ya michuano hiyo.

Akizungumzia ushindi huo mara baada ya kumalizika kwa fainali hiyo ya juzi, Saintfiet alisema maandalizi na kujituma kwa wachezaji wake ndio sababu kubwa ya kutetea vyema ubingwa huo.

"Wamecheza vizuri, mchezo ulikuwa mgumu nawapongeza wachezaji wangu wamepigana hadi tone la mwisho na kutwaa kombe hilo, ni mafanikio kwangu na klabu" alisema Saintfiet.

Aidha kocha huyo alisema wachezaji wake wameelewa mafunzo yake mapema na kujenga timu nzuri yenye ushindani muda wote.

"Hapa tumeanza vizuri nina imani tukiongeza bidii na kujijenga zaidi tutapata makombe zaidi likiwemo la Ligi Kuu ya Tanzania" alisema Saintfiet.

Aliongeza kuwa kuna makosa machache ambayo yameonekana kipindi hiki cha mashindano, atatumia muda uliobaki kurekebisha ili kupata timu itakayokuwa tishio kwenye ligi ijayo.

Tom aliwataka wachezaji wake watulie na waelekeze macho kwenye maandalizi ya ligi kuu jambo ambalo litawapa wakati mzuri kwa kuwa ligi itakuwa ngumu zaidi.

Yanga itakuwa kwenye mapumziko ya muda mfupi kabla ya kuanza rasmi maandalizi ya ligi hiyo msimu ujao wa 2012-2013 unaotarajiwa kuanza Septemba Mosi, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment