30 July 2012
Askofu Songea aonya viongozi
Na Joseph Mwambije, Mbinga
ASKOFU Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea, Kanisa Katoliki, mkoani Ruvuma, Mhashamu Norbert Mtega, amewataka viongozi nchini kuheshimu miiko ya uongozi tofauti na ilivyo sasa.
Mhashamu Mtenga aliyasema hayo jana katika katika Jubilei ya miaka 25 ya Jimbo la Mbinga na Jubilei ya miaka 25 ya utumishi wa Askofu mstaafu wa jimbo hilo Emanuel Mapunda.
Sherehe hizo zilihudhuliwa na viongozi mbalimbali ngazi ya Mkoa na kitaifa akiwemo Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu Bw. Benjamin Mkapa ambaye alikuwa mgeni rasmi, Kaimu Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Joseph Mkilikiti na maaskofu kutoka ndani na nje ya nchi.
“Uongozi bora ni ule unaofuata miiko ya uongozi na wanatoka kwa Mungu, jambo la msingi wanapaswa kuheshimu mfumo wa uongozi uliowekwa na sheria kwani bila mambo haya, nchi itayumba.
“Wananchi lazima tukubali kuongozwa kupitia viongozi waliopo na kuheshimu mfumo wa sheria, kama jamii inataka kufanikiwa lazima ikiri kuwa Mungu yupo kwani mataifa mengi ambayo yamemkana Mungu yameporomoka,” alisema Mhashamu Mtenga.
Akinukuu maneno yaliyopo kwenye kitabu cha Biblia, alisema hata shetani alikuwa malaika mwema mbele za Mungu lakini alipomkana na kuasi, alifukuzwa mbinguni hivyo aliwataka viongozi kutomkana Mungu.
Katika hatua nyingine, alisema neno linalomtaja Mungu kwenye
Katiba lisifutwe na kutahadhalisha kuwa, kama litafutwa Taifa litafutika kwani Mungu lazima atajwe kwani ndiye aliyefanikisha nchi kupata uhuru bila kumwaga damu.
Aliwataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya na kutaka masilahi binafsi yasipitishwe na kuwasihi waumini wa dhehebu hilo kufanya maombi ili mifumo bora ya uongozi ifuatwe kwani nchi haiwezi kuendelea bila kuwa na viongozi bora ambao ni zawadi ya Mungu.
Kwa upande wake, Bw. Mkapa aliwataka wananchi kutumia haki yao ya kimsingi ili kutoa maoni yao kuhusu Katiba Mpya ambayo ndio italeta, kulinda, kudhibiti haki, amani, upendo, umoja, mshikamano, utamaduni na kuvumiliana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment