23 July 2012

RC ajitosa kuwatetea wakulima wa korosho


Na John Gagarini, Pwani

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Bi. Mwantumu Mahiza, ametoa siku mbili kwa Chama cha Ushirika mkoani humo (CORECU), kumpa majina ya vyama vya msingi ambavyo havijawalipa wakulima wa zao la korosho msimu uliopita.


Bi. Mahiza aliyasema hayo juzi baada ya kutembelea ghala la kuhifadhi korosho za wakulima wa mkoani hapa na kuongeza kuwa,  ili kuondoa migogoro vyama hivyo vione umuhimu wa kuwalipa wakulima kwa wakati.

Alisema kati ya malamiko yaliyofikishwa kwake na wakulima hao ni pamoja na kutolipwa fedha za korosho walizouza msimu uliopita wakisubili ununuzi wa korosho awamu ya pili ambazo zipo katika maghala bila kujia hatma yao.

“Malalamiko mengine ni korosho kuchelewa kuuzika wakati msimu mwingine unakaribia wakitakiwa kuondoa kulosho iliyopo kwenye maghala ili yaweze kuwekwa dawa,” alisema Bi. Mahiza.

Aliongeza kuwa, vyama hivyo vimekopa fedha benki lakini jambo la kushangaza bado wameshindwa kuwalipa wakulima ambao wamepoteza nguvu kubwa kwa kilimo hicho.

“Wakulima wa korosho wanateseka kwa kukosa haki zao kutokana na vyama hivi kuweka vikwazo na kufanya uzembe unaosababisha Serikali kutupiwa lawama,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Bi. Mahiza alilazimika kutoa siku mbili akitaka majibu ya uhakika kutoka kwa Mrajisi Msaidizi wa Mkoa pamoja na Mwenyekiti wa CORECU na wakishindwa kufanya hivyo, watawajibishwa kwa kuhamishwa mkoa mwingine.

Akizungumza mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Mrajisi wa Mkoa Bi. Hadija Mangera, alisema walifanya ukaguzi wa mwezi mmoja na kubaini baadhi ya vyama vya msingi vimepoteza vitabu vya kumbukumbu na taarifa hazijitoshelezi.

Majibu hayo hayakumridhisha Bi. Mahiza ambaye alitaka kupatiwa vielelezo hivyo ili kujiridhisha kama wakulima hao wanapewa haki zao za fedha kwa asilimia 100.

Mkoa huo una jumla ya Vyama vya Msingi vya wakulima wa Korosho 88, ambavyo korosho zao bado hazijapata soko hivyo zimehifadhiwa katika ghala la Mbagala.

No comments:

Post a Comment