23 July 2012

Dkt. Shein aongoza dua waliokufa ajali ya meli


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein, jana ameungana na viongozi mbalimbali wa kitaifa katika dua maalumu ya hitma na sala (Salatul Mayyit al-ghaib), katika msikiti wa Mushawar, Mwembeshauri, mjini Zanzibar.

Sala na dua hiyo ni maalumu ili kuwaombea watu waliokufa kutokana na ajali ya kuzama kwa meli ya Mv Skagit, ambayo imetokea Julai 18 mwaka huu, wakati akitoka Dar es Salaam
kwenda Zanzibar na kusababisha vifo, majeruhi kadhaa.

Taarifa iliyotolewa na Mwandishi wa Rais, Ikulu Zanzibar jana, Bw. Rajab Mkasaba, imesema sala na dua hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini, vyama na Serikali.

Viongozi hao ni pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muunganao wa Tanzania, Dkt. Mohammed Kharib Bilal, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd na Rais mstaafu wa Zanzibar, Dkt. Amani Abeid Karume.

Wengine ni Mufti Mkuu wa Zanzibar, Shekhe Omar Khabh, Kadhi Mkuu wa Zanzibar, Shekhe Khamis Haji, Spika wa Baraza la Wawakishi Bw. Pandu Ameir Kificho, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharib Bw. Abdalla Mwinyi Khamis, Mawaziri, Manaibu Waziri, Wabunge, Wawakilishi, Mashekhe mbalimbali wa Zanzibar na Tanzania Bara, wananchi na viongozi wengine.

No comments:

Post a Comment