05 July 2012

Polisi wadaiwa kuvunja milango, madirisha Bukoba



Na Livinus Feruzi, Bukoba

WAKAZI wa Kata ya Kahororo, Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, wamelalamikia kitendo cha Jeshi la Polisi mkoani hapa kuvamia makazi yao saa sita usiku, kuvunja milango pamoja na madirisha ya nyumba zao bila sababu za msingi.


Polisi hao ambao walivaa kiraia, wanadaiwa kuvamia nyumba hizo ili kuwasaka watu wanaohusika na mgogoro wa ardhi uliopo kati ya wananchi na mmiliki wa Shule ya Sekondari Nyanshenye.

Wakizumgumza na waandishi wa habari, wakazi hao walisema tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia juzi ambapo baadhi ya wananchi walikamatwa na kupelekwa kituoni.

“Uvamizi huu na kukamatwa kwa baadhi ya wakazi wa kata hii, kunatokana na mgogoro wa ardhi ambao umedumu muda mrefu tangu mwaka 1986 baada ya shule hiii binafsi kuvamia ardhi ya wananchi kila mmoja akidai ni ardhi yake,” alisema mkazi mmoja wa kijiji hicho (jina tunalo).

Mkazi mwingine wa eneo hilo, anayeishi mtaa wa Kyaya (jina tunalo), alisema kitendo cha polisi kuvamia makazi yao wakiwa wamelala, kiliwafanya wananchi washindwe kuwatofautisha polisi hao na kikundi cha majambazi.

“Kama hawa polisi walikuwa na dhamira ya kuwatafuta watu waliovunja nguzo za shule, kwanini walishindwa kupitia kwa uongozi wa Serikali ya Mtaa.

“Mimi nilishangaa kusikia watu wanagonga mlango nyumbani kwangu kama majambazi lakini nilipoamka na kuwachungulia, niligundua ni polisi ambao baadhi yao walivaa sare, nilipouliza wanataka nini wakasema wanamtaka mke wangu,” alisema.

Akizungumzia madai hayo, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Philip Kalangi, alikiri wananchi kuvamiwa na kukamatwa kwa madai kuwa, watu hao walikuwa wakitafutwa muda mrefu.

“Watu waliokamatwa walikuwa wakitafutwa tangu Machi mwaka huu baada ya kupewa dhamana na kushindwa kurudi,” alisema Kamanda Kalangi.

Kauli hiyo ilipingwa vikali na wananchi na uongozi wa mtaa huo ambao ulisema hakuna mwananchi aliyekamatwa wala kupewa dhamana kama inavyodaiwa.

“Siwezi kuzungumzia tuhuma za polisi kuvunja milango na madirisha kwa sababu sina taarifa nazo, nipeni muda niendelee kufuatilia ili kujua ukweli wake,” alisema Kamanda Kalangi.

No comments:

Post a Comment