16 July 2012
Ndoa ya Dk. Slaa yapingwa kortini *Mkewe afungua kesi Mahakama Kuu Dar *Ilikua ifungwe Julai 20 na mchumba wake *Adaiwa kutelekeza familia yake, ataka fidia
Na Rehema Mohamed
PAMOJA na Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuwa na dhamira ya kufunga ndoa na mchumba wake Bi. Josephine Mshumbusi, mke wa Katibu huyo Bi. Rose Slaa, amefungua kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaa kupinga kusudio la mumewe.
Katika kesi hiyo namba nne ya 2012, ambayo imefunguliwa mahakamani hapo Julai 5 mwaka huu, Bi. Slaa anadai, Dkt. Slaa bado ni mumewe wa ndoa na kudai fidia ya sh. milioni 550.
Kati ya fedha hizo, sh. milioni 50 ni kwa ajili ya gharama za malazi na malezi ya familia yake, watoto wawili aliozaa nae na kuiomba Mahakama itoe amri kwa Bi. Mshumbusi, amlipe sh. milioni 500 kwa uzinzi na kusababisha Dkt. Slaa alete athari kwake na familia yake kwa ujumla.
Kwa mujibu wa hati ya kesi hiyo, ndoa ya Dkt. Slaa na Bi. Mushumbusi inatarajiwa kufungwa Julai 21 mwaka huu, mjini Karatu, mkoani Arusha.
Bi. Slaa pia aliiomba Mahakama itoe amri kwa Dkt. Slaa na Bi. Mshumbusi kuwa, wote hawana vigezo vya kuoana kwa sababu yeye bado ni mke halali wa Katibu huyo.
Katika hati hiyo, Bi. Slaa anadai ndoa anayotarajia kufunga Dkt. Slaa na Bi. Mushumbusi ni batili kwani uhusiano wao ulikuwa bado unaendelea.
Alidai yeye na Dkt. Slaa walikuwa na uhusiano tangu mwaka 1985 ambapo Juni 18,1987 walifanikiwa kupata mtoto wa kike aliyemtaja kwa jina la Emiliana Slaa na kuambataniha kopi ya cheti chake cha kuzaliwa namba 0518970, kama sehemu ya ushahidi wake.
Aliongeza kuwa, Septemba 23,1988 walibahatika kupata mtoto mwingine wa kiume anayeitwa Linus Slaa ambapo yeye na Dkt. Slaa walikuwa wakiishi katika nyumba moja kama mke na mume.
Bi. Slaa alisema katika maisha yao, taratibu zote zinazohusu utamaduni wa ndoa zilifuatwa kwa familia zao na walitambulika kama mke na mume.
Ilielezwa kuwa, katika kipindi hicho waliishi kwa amani, upendo na kupanga mikakati ya baadaye ya familia yao na walifanikiwa kununua nyumba Sinza, kitalu namba 609 Block E.
Pia walinunua kiwanja cha makazi katika Kijiji cha Gongali, kilichopo Wilaya ya Karatu, mkoani Arusha, kujenga nyumba mwaka 2005 pamoja na kununua thamani za ndani.
Aliongeza kuwa, uhusiano wao ulianza kulega mwaka 2009 baada ya Dkt. Slaa kuanza uhusiano na Bi. Mshumbusi hivyo kuisaliti ndoa yao kwa kulala nje na kutumia vibaya mali za familia kwa kuishi maisha ya hanasa na mwanamke huyo.
Alisema mahusiano ya Bi. Mshumbusi na Dkt. Slaa, yaliendelea hadi kufikia hatua ya kutokuwa na siri tena kati yao kwa ndugu zake, viongozi wa kanisa, waumini na jamii nzima, walishuhudia na baadaye kusambaa katika vyombo vya habari.
Alidai Dkt. Slaa alimtangaza Bi. Mshumbusi kwenye jukwaa la siasa jambo ambalo lilimuathiri kisaikolojia ambapo tangu mwaka 2009, Katibu huyo aliitelekeza familia yake hivyo yeye kubeba majukumu yote ya kifamilia pamoja na kuwatunza watoto wao kwa chakula, malezi, malazi na ada za shule.
Alisema mtoto wao Emilian alikuwa akisoma Chuo Kikuu cha Ardhi na Linus anasomea Stashahada ya masuala ya kompyuta katika chuo cha DIT. Aliongeza kuwa, wakati akifanya jitihada kwa wazee na viongozi wa kanisa ili wamkutanishe na Dkt. Slaa kwa ajili ya usuluhisho wa mgogoro wao, Katibu huyo na Bi. Mshumbusi wametoa tangazo la ndoa itakayofungwa Julai 21 mwaka huu.
Anadai pamoja na Dkt. Slaa kuchukua uamuzi wa kuoa mwanamke mwingine, hakuweka wazi maisha ya baadaye ya familia yake na haki za msingi za mke wake.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa mbele ya Jaji Laulence Kaduri ambapo leo itakuja kwa ajili ya kutajwa. Bi. Slaa anawakilishwa na wakili Bi. Joseph Tadayo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment