16 July 2012
Bodi ya Maghala yapunguza upotevu wa mazao ya kilimo
Na Reuben Kagaruki
BODI ya Leseni za Maghala nchini (TWLB), imesaidia kupunguza upotevu wa mazao ya wakulima kabla ya kumfikia mlaji kutokana na elimu wanayotoa kuhusu njia bora za ufungashaji.
Akizungumza na Majira Dar es Saklaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Bi. Elizabeth Kimambo, alisema kuanzishwa kwa TWLB kumechangia kuongeza wingi wa mazao tofati na wakati ambao ilikuwa haijaanzishwa.
Alitolea mfano kuwa, wakati bodi hiyo inaanzishwa 2007/08, uzalishaji wa korosho mkoani Mtwara peke yake ulikuwa tani 55,000, hivi sasa umeongezeka nchi nzima na kufikia 158,000.
Alisema siri ya mafanikio ni kutokana na bodi kuwajibika kuwatafutia wakulima masoko ya mazao yao ambayo yamehifadhiwa kwenye maghala.
“Hii inatokana na wakulima kuridhika na bei wanayopata na kuwawezeshwa kupata mikopo kutoka taasisi za fedha kwa kutumia dhamana ya mazao waliyohifadhi kwenye maghala.
“Wakulima walionufaika na mikopo ya aina hii ni wale wa mikoa ya Mtwara, Lindi, Pwani, Ruvuma na Tanga, mafanikio wanayopata kwa kuhifadhi mazao yao kwenye maghala, yamechochea ongezeko la tani za kurosho kutoka 55,000 hadi 158,000.
Alisema kutokana na hali hiyo, mkulima anaweza kuendesha maisha yake kwa mkopo aliopata kwa dhamana ya mazao hata kabla ya mauzo ambapo suala la upotevu wa mazao, asilimia 40 yanapotea kabla ya kumfikia mlaji kutokana na ufungashaji duni.
Bi. Kimambo alisema anaamini tatizo hilo lilikuwa kubwa zaidi ya hapo, lakini hivi sasa limepungua sana kutokana na elimu ambayo wamekuwa wakiitoa.
Bodi hiyo ilianzishwa nchini mwaka 2007 ambapo hadi sasa ina maghala zaidi ya 40 yaliyo chini yao na kutoa mwito kwa kampuni zenye mpango wa kuanzisha maghala, kuwasiliana na bodi hiyo ili kupata maelekezo ya kina.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment