16 July 2012
Madaktari wazidi kutunisha misuli *Kufukuzwa kwao hakuwatishi, Ulimboka aanza kutembea
Stella Aron na Rehema Maigala
JUMUIYA ya Madaktari nchini, imesema hatua ya Baraza la Madaktari Tanganyika, kusitisha usajili madaktari 390 kwa sababu ya kushiriki kwenye mgomo, si njia ya kumaliza tatizo lililopo ambapo uamuzi huo waliutarajia na hauwashtushi.
Katibu wa jumuiya hiyo, Dkt. Edwin Chitage aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya hatua ya baraza hilo kusitisha kwa muda usajili wa madaktari walioshiriki mgomo.
Alisema usitishwaji wa usajili huo, hautawafanya washindwa kuomba kazi katika taasisi zingine kwani kati ya madai ya msingi ambayo waliyapeleka serikalini ni pamoja na kutokubaliana na mfumo wa utendaji wa baraza hilo.
“Kimsingi tulitarajia baaraza litatoa uamuzi huu lakini hautishtui kwani madaktari wana uwezo wa kuomba kazi katika taasisi zingine,” alisema Dkt. Chitage na kuongeza kuwa, Mwenyekiti wa baraza hilo ndiye Mganga Mkuu wa Serikali, hivyo ana haki ya kuitetea Serikali na ndiye anayesimamia mambo yote.
Aliongeza kuwa, Mganga Mkuu wa Serikali kuwa Mwenyekiti wa baraza, kunasababisha madaktari kukosa uhuru wa kujadili kasoro mbalimbali zilizopo katika sekta hiyo.
Hata hivyo, Dkt. Chitage alisema tangu juzi, kumekuw na fukuto la kuanza tena kwa mgomo wa madaktari kutokana na kitendo cha kiongozi wao kufikishwa mahakamani.
Viongozi wa dini
Wakati huo huo, viongozi wa dini waliotoa tamko la kuikaanga Serikali kwa kushindwa kumaliza mgomo huo na kuonekana kuwa upande wa madaktari, jana wametoa tamko jingine la kutishia kuwaburuta wataalam hao mahakamani kwa madai kuwa, wamesababisha vifo vya wagonjwa kipindi cha mgomo.
Msemaji wa Kamati ya Vijana ya Baraza Kuu la Waislamu nchini (BAKWATA), Shekhe Saidi Mwaipopo, alisema baraza hilo linakusudia kuwaburuta mahakamani kwa makosa ya mauaji.
Alisema waliamua kuingilia kati suala hilo kwa sababu jukumu moja wapo walilonalo ni upatanisha ambapo Rais Jakaya Kikwete alikubali kukutana na viongozi hao kwa sharti la kuwataka madaktari waliogoma kuandika barua ya kuomba radhi.
Kauli hiyo inaonekana kupingana na taarifa iliyotolewa na Ikulu ambayo ilieleza kuwa, mjadala wa suala hilo umeshafungwa na Serikali haipo tayari kukutana nao.
“Tulipokutana nao na kuwataka waandike barua ya kuiomba radhi Serikali, walikataa hivyo kwa msimamo huo tunaamini kuna jambo wanaloliamini na sisi hatupo upande wowote,” alisema.
Shekhe Mwaipopo aliwalaumu madaktari hao kwa hatua ya kuomba ulinzi Umoja wa Mataifa (UN) kwa ajili ya Dkt. Steven Ulimboka, hali inayoonesha dhahiri kuwa hawana imani na Serikali na vyombo vya ulinzi hivyo wanaandaa maelezo kwa kushirikiana na mawakili ili kupata ya idadi ya watu waliokufa wakati mgomo huo.
Akijibu tuhuma hizo, Dkt. Chitage alisema wameshangazwa na kauli alizotoa Shekhe Mwaipopo kwani wao waliamini watu waliokuwa wakizungumza nao, walikuwa na nia ya kutatua mgogoro huo.
“Hawa walikuja kwa gia ya kuzungumza na sisi kwa moyo wa Kimungu wanaomtumikia kumbe wana ajenda ya siri, sisi hatupo tayari kuomba radhi,” alisema Dkt. Chitage.
Hali ya Dkt. Ulimboka
Wakati huo huo, Dkt. Chitage alizungumzia hali ya Dkt. Ulimboka na kudai kuwa, inaendelea vizuri na amenza mazoezi ya kutembea.
“Kwa kweli tunamshukuru Mungu, hali ya Dkt. Ulimboka awali ilikuwa mbaya lakini hivi sasa anaendelea vizuri, ameanza kufanya mazoezi ya kutembea na anaweza kuongea,” alisema
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment