05 July 2012

Muungano waibua hoja nzito bungeni *Upinzani wataka historia yake iwekwe hadharani *Wadai itasaidia kuwaondoa hofu Watanzania wote



Na Benedict Kaguo, Dodoma

KAMBI ya Rasmi ya Upinzani Bungeni, imesema historia halisi ya Muungano uliopo, imekuwa ikifichwa licha ya ahadi za mara kwa mara juu ya elimu itakayotolewa kwa umma kuhusu jambo hilo.

Msemaji wa kambi hiyo, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano, Bw. Tundu Lisu, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati akiwasilisha maoni ya kambi hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/13.


Alisema zaidi ya tendo la kuchanganya udongo na matukio mengine yaliyofanyika hadharani, Watanzania wengi hawafahamu historia halisi ya Muungano huo.

Aliongeza kuwa, kambi hiyo inashauri kuwa, umefika wakati wa Serikali kuweka wazi nyaraka mbalimbali zinazohusu historia ya Muungano na mapito yake ili Watanzania waelewe masuala yote yaliyojitokeza wakati huo.

“Hii ni muhimu zaidi kwa kutokana na ukweli kwamba, Mataifa ya Magharibi kama Marekani na Uingereza, yalishatoa hadharani nyaraka za mashirika yao ya kijasusi ambapo Balozi zao nchini zinaonesha Serikali zao zilivyohusika kuzaliwa Muungano huu.

“Kuanikwa kwa nyaraka zilizoko katika mamlaka mbalimbali za Serikali, kutasaidia kuthibitisha au kukanusha taarifa ambazo chanzo chake ni nyaraka za kidiplomasia na kijasusi.

“Zipo taarifa zinazodai Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, ulitokana na njama za kibeberu kudhibiti ushawishi wa siasa za kimapinduzi za chama cha umm na viongozi wake ndani ya Baraza la Mapinduzi wakati huo,” alisema Bw. Lissu.

Alisema nyaraka hizo zitatoa mwanga juu ya kilichowasibu viongozi waandamizi wa chama hicho ambao bila uwepo wao kutambuliwa rasmi, historia ya Mapunduzi ya Zanzibar na Muungano inakuwa na kasoro kwani miaka 50 ya Muungano ni umri wa kutosha kwa Taifa la Tanzania kuambiwa ukweli wote juu ya kuzaliwa kwake na mapito ambayo limepitia katika kipindi hicho.

Hata hivyo, Bw. Lissu alisema mambo yote katika orodha ya mambo ya Muungano baada ya mwaka 1964, yalikuwa nje ya makubaliano na Sheria ya Muungano hivyo yalikuwa batili

No comments:

Post a Comment