19 July 2012

Mume, mke wadaiwa kuua mtoto mchanga


Na Joseph Mwambije, Songea

JESHI la Polisi mkoani Ruvuma, linawashikilia watu wawili mke na mume ambao wanatuhumiwa kumuua mtoto wa miezi saba kwa kumpiga na mawe, kumuweka katika mtaro wa maji kutokana na tofauti za kimapenzi zilizojitokeza kati yao.

Akizungumza na Majira, Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Chemchem, Kata ya Matogoro, mkoani hapa, Bw. Fama Suta, aliwataja  watuhumiwa hao kuwa ni Bw. Shangwe Komba (28) na Bi. Mwazani Chimgege (25), wakazi wa mtaa huo.

Alisema tukio hilo lilitokea mtaani hapo Julai 16 mwaka huu na taarifa zimetolewa Kituo cha Polisi Mjini Kati.

Akielezea mazingira ya tukio hilo, Bw. Suta, alisema mtoto huyo ambaye hajazaa na Bw. Komba, alinyweshwa sumu kabla hajauawa na kuliiita tukio hilo la kinyama lisilostahili kuvumiliwa.

“Awali polisi walimkamata dada wa Bw. Komba ambaye anaitwa Bi. Zawadi Komba na kufanya naye mahojiano juu ya tukio hili lakini yeye alisema kuwa, mdogo wake alimuomba sh. 50,000 akamtibu mwanae wa kufikia (marehemu),” alisema Bi. Komba.

Alisema baada ya kumpa pesa hiyo, alirudi kwa mara nyingine na kwenda kuomba pesa lakini Bi. Komba alimjibu kuwa, kama atalazwa ndio atampa pesa nyingine.

Inaelezwa kuwa, baada ya mtuhumiwa kupewa majibu hayo na dada yake, aliamua kueleza ukweli kuwa anaomba pesa hizo kwa sababu amemuua mwanae hivyo anataka kukimbia.

“Kwa kweli inaonesha ni jinsi gani huyu mwanaume alishauriana na mkewe wamuue mtoto ili wafurahie maisha na kutafuta mtoto mwingine ambaye watamzaa wao,” alisema Bw. Suta.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Deudediti Nsemeki, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa, uchunguzi unaendelea ili kubaini chanzo chake kalba ya watuhumiwa kufikishwa mahakamani.

No comments:

Post a Comment