16 July 2012
Mkapa aiwakilisha Tanzania mkutano wa kimataifa China
Na Imma Mbuguni, Suzhou, China
MKUTANO mkubwa uliolenga kuimarisha uhusiano kati ya nchi za Afrika na China, umemalizika jana katika mji wa Suzhou, ambapo mada mbalimbali zilizojadiliwa, ziliibua hizia za washiriki wengi.
Baadhi ya viongozi walioshiriki mkutano huo ni pamoja na marais wastaafu, Bw. Joachim Chisano (Msumbiji), Bw. Olusegun Obasanjo (Nigeria), Bw. John Kufor (Ghana), Bw. Dihab (Sudan), pamoja na Bw. Sivestor wa Burundi.
Mkutano huo ulifunguliwa juzi na Makamu wa Rais wa China, Bw. Xin jin Ping, ukiwa na kauli mbiu inayosema “Sauti za watu, urafiki na ushiriki kwa ajili ya watu”, ambapo Tanzania iliwakilishwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa.
Mategemeo ya washiriki wa mkutano huo ni kuimarisha uhusiano wa nchi zao na China ili kuchochea maendeleo ya haraka ambapo Afrika ina uwezo wa kujitegemea ili kufikia maendeleo na China inaweza kujifunza mengi kutoka Afrika.
Wajumbe wa mkutano huo hawakusita kueleza jinsi Afrika inavyoweza kufanikiwa katika suala la demokrasia na kuchagua viongozi wao kwa kutumia mifumo bora.
Hata hivyo, wajumbe hao walidai kuwa, pamoja na demokrasia nzuri iliyopo katika nchi mbalimbali za Afrika, bado haijaendelea. Mmoja wa wajumbe aliyeongoza mjadala Profesa Li Honwu, alisema kuwa demokrasia ya kweli lazma ianzie katika mahitaji ya kweli.
Prof. Honwu ambaye ni Mtafiti wa Masuala Maalumu ya Afrika, alizitaka nchi hizo kutoyumbishwa ili kufikia maendeleo ya haraka zaidi kuliko mataifa mengine duniani.
Katika ufunguzi wa mkutano huo, Makamu wa Rais Bw. Ping aliwashukuru viongozi wa Afrika kwa kuendeleza uhusiano mzuri na kusisitiza kuwa, mikakati mipya na endelevu inatakiwa ili kuhimarisha zaidi uhusiano uliopo.
Alisema mahusiano ya nchi za Afrika na China kibiashara, yamesaidia kukuza pato la nchi hadi kufikia dola za Marekani bilioni 14.9 na limeongeza ajira Afrika, kuimarisha huduma pamoja na mawasiliano.
Leo wajumbe wa mkutano huo watapata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali nchini hapa ili kujionea maendeleo yaliyofikiwa na nchi hiyo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment