20 July 2012

Milovan awaponda washambuliaji wake



Na Elizabeth Mayemba

KOCHA Mkuu wa Simba, Milovan Cirkovic amesema pamoja na timu yake kucheza vizuri bado kuna tatizo kubwa katika safu ushambuliaji.

Simba juzi iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Ports ya Djibouti, baada ya awali kufungwa na URA ya Uganda mabao 2-0.


Miamba ya soka nchini, Simba na Yanga wamejikuta wakiibukia kwa vibonde ambapo Yanga waliifunga Walau Salaam ya Sudan Kusini kwa mabao 7-1 lakini mechi ya kwanza walipigwa mabao 2-0 na Atletico ya Burundi, lakini zote kwa pamoja zimetinga hatua ya robo fainali.

Akizungumza Dar es Salaam juzi mara baada ya kumalizika mchezo dhidi ya Ports, Kocha Mkuu wa Simba Milovan alisema timu yake bado ina tatizo katika safu ya ushambuliaji.

"Hata ukiangalia mechi ambayo tulifungwa na URA, tulipoteza nafasi nyingi sana ndivyo ilivyokuwa na kwa Ports kwani tulipoteza nafasi nyingi za kufunga ilikuwa tushinde zaidi ya mabao matano," alisema Milovan.

Alisema ana kazi kubwa ya kuhakikisha anafanyia marekebisho kikosi chake katika eneo hilo la ushambuliaji, ili mechi yao na Vita ya Congo waweze kufanya vizuri.

Milovan alisema hamu yake kubwa ni kuona timu yake inacheza fainali ya michuano hiyo na hatimaye kutwaa kombe, lakini kama wachezaji wake wataendeleza uzembe watajikuta wakiwa wasindikizaji tu katika michuano hiyo.

No comments:

Post a Comment