23 July 2012

Milovan aihofia Azam FC Kagame Cup


Na Speciroza Joseph

BAADA ya kuingia robo fainali ya Kombe la Kagame, kocha wa Simba, Milovan Cirkovic amesema kukutana na Azam FC kunawapa wakati mgumu wa kuendelea na mashindano hayo.

Simba juzi ilitoka sare ya bao 1-1 na AS Vita Club ya Congo DRC, kwenye mchezo wa makundi uliomalizika hivyo watakutana na Azam FC kwenye mchezo wa robo fainali, utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Akizungumza mara baada ya kupata taarifa za kuwa watacheza na Azam FC, Milovan alisema wanahitaji maandalizi ya nguvu na ya kutosha kwa kuwa timu hiyo si ya kubeza.

"Utakuwa mchezo mgumu sana kuliko michezo tuliyocheza, bila kufanya maandalizi makali tunaweza kupoteza ushindi," alisema Milovan.

Milovan aliongeza kuwa kwa wiki tatu wanakutana na Azam FC kwa mara ya tatu anaijuia timu hiyo, hivyo wanajiandaa kuweza kushinda na kuingia hatua ya nusu fainali ya mashindano hayo.

Akielezea mchezo wao na AS Vita, kocha huyo alisema timu yake ilikosa nafasi nyingi na muda mwingine walionekana kupumzika hali iliyosababisha kupata sare hiyo ya bao 1-1.

Alisema makosa yaliyoonekana kwenye mchezo huo yatarekebishwa mapema, kabla ya kucheza mchezo wa robo fainali kwa kuwa ni lazima wapate ushindi.

Simba wiki iliyopita kabla ya kuanza mashindano ya Kagame, walikutana na Azam FC kwenye fainali ya Kombe la Urafiki Tanzania ambapo Simba walitwaa ubingwa huo kwa kuifunga Azam FC kwa mikwaju ya penati ya 3-1.

No comments:

Post a Comment