23 July 2012

Yanga, Mafunzo vitani leo



Na Speciroza Joseph

MASHINDANO ya Kombe la Kagame, leo yanaingia hatua ya robo fainali ambapo bingwa mtetezi Yanga, atacheza dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo utakuwa wa pili, baada ya kumalizika wa mchana utakaozikutanisha URA ya Uganda itakayocheza na APR ya Rwanda.


Yanga itacheza mchezo huo ikiwa na ari ya kutaka kutetea kombe lao, tangu kuanza kwa mashindano hayo Yanga imepoteza mchezo mmoja na kushinda michezo miwili.

Timu hiyo ilifungwa mabao 2-0 na Atletico, ikapata ushindi wa mabao 7-1 dhidi ya El- Salaam Wau wa Sudan Kusini, kabla ya kuifunga APR mabao 2-0 katika michezo ya hatua ya makundi.

Mafunzo timu ngeni katika mashindano hayo, inasaka rekodi ya kumtoa bingwa mtetezi na kuingia nusu fainali kwa mara ya kwanza, katika michezo yake ya hatua ya makundi haijapoteza wala kufungwa mchezo wowote, imetoka sare michezo yote miwili dhidi ya Azam FC na Tusker ya Kenya.

Endapo timu mojawapo kati ya hizo itashinda itakutana na mshindi wa mechi kati ya URA na APR, katika mchezo wa nusu fainali ya kwanza utakaochezwa siku ya mbili zijazo.

Robo fainali nyingine zitachezwa kesho, ambapo mchezo wa kwanza utakuwa kati ya Atletico Olympique ya Burundi, dhidi ya AS Vita Club ya Congo DRC.

Mchezo wa pili utakuwa kati ya Azam FC na Simba zote za Tanzania, mshindi wa mchezo huo atacheza dhidi ya mshindi kati ya Atletico na AS Vita Club.

No comments:

Post a Comment