10 July 2012

Migomo ya wafanyakazi yapigwa marufuku


Na Goodluck Hongo

SERIKALI imepiga marufuku migomo sehemu za kazi na kuwataka wafanyakazi kufuata sheria na kanuni zilizopo ili kudai haki zao.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Kamishna Msaidizi wa Kazi kutoka Wizara ya Kazi na Ajira Bw. Josephat Lugakingira, alisema hivi karibuni kumekuwa na vitisho vya migomo isiyozingatia taratibu zilizopo kisheria.


Alisema kwa mujibu wa kifungu cha 80(1) cha Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini namba 6/2004, ili mgomo uwe halali lazima uzingatie mambo muhimu ikiwemo mgogoro wa kimasilahi kati ya mwajiri na wafanyakazi.

“Kwa mijibu wa kifungu cha 76(1) cha sheria hiyo, wafanyakazi walio katika huduma muhimu hawaruhusiwi kugoma isipokuwa baada ya kukidhi vigezo kadhaa vinavyosimamiwa na kamati ya huduma muhimu.

“Kimsingi migomo sehemu za kazi inaathiri nchi kiuchumi ambapo waathirika wakubwa ni wananchi,” alisema Bw. Lugakingira.

Akizungumzia tishio la mgomo wa walimu kupitia Chama cha Walimu Tanzania (CWT), mkoani Geita, Bw. Lugakingira alisema mgomo huo ni batili kwa sasabu madai yao yaliwasilishwa katika tume ya usuluhishi na uamuzi  yenye namba za usajili CMA/DSM.ILA/369/12.

“Tume inaendelea kushughulikia madai yao, tunachukua fursa hii kuwajulisha wafanyakazi wote kuwa migomo ambayo si halali ina madhara yake pamoja na kuchukuliwa kwa hatua za kinidhamu dhidi ya wahusika.

“Tunawaomba wafanyakazi wasijihusishe na vitendo vya uvunjaji sheria badala yake sheria na kanuni zinazotawala mahusiano sehemu za kazi ziheshimiwe na kuzingatiwa,” alisema.

Hivi karibuni, CWT mkoani humo kupitia chombo kimoja cha habari, walitangaza azimio la kufanya mgomo usio na kikomo lakini Bw. Lugakingira alisema madai yao si halali.

“Wao wanapaswa kusema mambo ambayo Serikali imeyatekeleza kwao na mangapi hayajatekelezwa ili Watanzania wafahamu kwani kila siku yanaibuka madai mapya kana kwamba Serikali haijawahi kutekeleza madai yao yoyote,” alisema.

1 comment:

  1. Waacheni wagome muwafukuze kazi kwa sasa wengi hatuna ajira. acheni kuhangaikia mambo yasiyo na umuhimu,anayeona mshahara haumtoshi aondoke akapate huko kwingine mshahara anaoutaka

    ReplyDelete