10 July 2012

Kampeni ya kutokomeza mauaji ya albino na vikongwe kumalaiza janga hilo



Na Mwandishi wetu

KATIKA jamii kila mwanadamu ana wito au kipaji ambacho amepewa na mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuwahudumia jamii katika masuala mbalimbali.

Matukio mengi ya mauaji na ukatili yanayotokea sasa ni nchini ni kutokana na ukosefu wa maadili miongoni mwetu ambapo baadhu ya watu wamekosa ubinadamu kwa wenzao.

Vitendo hivyo vimeendelea kutokea na kutishia uhai wa raia wasio na hatia watoto wamekuwa wakiuawa kwa imani za kishirikina huku watu wenye ulemavu wa ngozi wakiendelea kukatwa viungo vyao.

Rushwa, ufisadi katika nchi nyingi za Afrika leo ni kutokana na ubinafsi ambao ni adui mkubwa wa maendeleo, visipokemewa na viongozi mbalimbali wakiwemo wa dini vinaweza kuangamiza Taifa.

Kati ya watu ambao wamekuwa wakitumia vipaji hivyo ni Askofu wa Jimbo la Shinyanga wa Kanisa la Field Evangelism Askofu Edson Mwombeki.

Licha ya kufanya kazi ya kueneza neno la Mungu pia ameamua kujikita katika suala mauaji ya albino, vikongwe na utoaji wa misaada kwa maskini.

Pamoja na matatizo mbalimbali yanayowakumba vikongwe na albino dhidi ya imani za kishirikina hasa katika Mkoa wa Shinyanga ameamua kuzindua kampeni ya kuhakikisha elimu inawafikia wananchi na kuondokana na dhana potofu za kishirikina.

Anasema anaamini kwamba vikongwe wenye macho mekundu si wachawi hivyo wanahitaji misaada ikiwa ni pamoja na kuwa nao karibu hata kwa kuandaa chakula nao na kula nao ili kujiona kuwa wapo sawa na watu wengine.

Anasema kuwa, huduma yake ya kutaka kuwafikia maskini ni wito ambao uko ndani lengo likiwa kuhakikisha maskini wote wanapata mabadiliko ambapo kazi hiyo ndiyo aliyokuwa akiifanya Yesu kwa kuwapelekea wahitaji habari njema au kwa lugha nyingine ni maskini.

Anasema kuwa mfumo wa sasa ni kuwa wachungaji na maaskofu wengi hawana mwako wa kupanga mikakati ya kuwafikishia habari njema maskini na kusababisha kuachwa kwa kundi kubwa likiteseka pasipo msaada wowote.

"Ukweli injili ni kuhakikisha maskini wanafikiwa na habari njema ili nao waweze kubadilika waweze kutoka katika umaskini na kuwa watu waliokombolewa kifikra na kuwekwa huru na kuuaga umaskini wa kiroho, " anasema askofu Mombeki.

Anasema kuwa kanisa hilo hivi sasa lina changamoto ya kuhakikisha kuwa watu wenye kipato kidogo wanasaidiwa na kuweza kujishughulisha kwa biashara ndogo ndogo ili waweze kujikwamua kimaisha.

"Jukumu la kanisa ni kuhakikisha umaskini ni kuwapatia elimu ya kukabiliana na changamoto za maisha hivyo waumini wetu wana kazi ya kuwafundisha namna ya kujikwamua kwa kufanyakazi kwa bidii ili waondokane na adha hiyo," anasema askofu Mombeki.

Anasema alianza huduma ya kuwafikia maskini na vikongwe mwaka 2005 mkoani humo kwa kuwapatia chakula watoto wa mitaani na ombaomba kilichogharimu shilingi 13,0000.

"Niliendelea kula chakula na wahitaji yaani vikongwe, albino pamoja na ombaomba wa mitaani kila jumamosi hali ambayo ukifika mkoani na kuwafanya wajikusanye zaidi baada ya kupata msada huo,"

Mbali na chakula pia hufundushwa namna ya kufanya kazi na kuvunja fikra potofu ya kuamini kuwa wao ni maskini ambapo wengi wamebadilika na kuamua kufanya wakijipatia kipato kwa njia ya kufanya kazi likiwepo suala la kuwafundisha masuala ya kiroho.

"Kwa sasa tunakula chakula kwa mwezi mara moja ambapo watu kati ya 400 mpaka 500 huwa tunakulanao chakula, kwa kuwa binadamu wote ni sawa, hatubagui dini ya mtu watu wote wamekuwa wakishiriki hafla hizo ambazo hufanyika kwa sasa mara moja kwa mwezi," anasema.

Mbali na kula chakula na wahitaji, vikongwe pamoja na albino kwa imani za kishirikina kanisa hilo pia limezindua kampeni inayoendelea kwa kutoa elimu kwa jamii kupitia mikutano mbalimbali inayoendeshwa na vyombo vya habari kuhakikisha jamii inaepukana na zana potofu kuwa vikongwe ni wachawi likiwepo suala la kuamini watu wanaweza kutajirika kwa kuua albino.

Anasema, wameendelea kuelimisha jamii na kusaidia kupunguza kasi ya mauaji ya vikongwe ambapo mpaka sasa hali imebadilika na kurudisha amani ya awali kwao.

Anasema, wanaamini katika kuliombea Taifa ambapo kila siku suala linaloombwa ni kuendelea kuwapo kwa amani iliyopo na kuzuia umwagaji damu.

"Miaka 12 ya kuwarudisha kondoo ni njia ya mungu kutaka kupata mtu atakayefundisha maadili nchini  ambayo ni chanzo cha kuogopa kula rushwa na kudhulumu wengine," anasema.

No comments:

Post a Comment