19 July 2012

Meli nyingine yazama Z'bar *Ilikuwa ikitoka Dar, 12 waripotiwa kufa, wapo watalii *130 waokolewa, utambuzi maiti kufanyika Maisara *Yadaiwa ilibeba abiria wengi kupita uwezo wake



Mwajuma Juma, Zanzibar na Anneth Kagenda, Dar

WATU 12 waliokuwa wakisafiri na meli ya Mv Scarget kutoka Dar es Salaam kwenda Zanzibar, wamekufa na wengine 130 kuokolewa baada ya meli hiyo kuzama Kusini mwa kisiwa cha Chumbe, visiwani Zanzibar.

Taarifa za uhakika ambazo zimelifikia gazeti hili hadi jana saa 12 jioni, zilisema idadi ya waliokufa katika ajali hiyo inatarajiwa kuongezeka kutokana na meli hiyo kuzama kabisa kwenye maji hivyo kutoonekana katika uso wa bahari.


Maiti zilizofikishwa nchi kavu jana jioni ni pamoja na watoto watatu wa kiume na wanawake wanne akiwemo mzungu mmoja.

Habari za kuzama kwa meli hiyo, zilithibitishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Dkt. Mwinyihaji Makame Mwadini, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Watu waliokolewa walifikishwa katika bandari ya Zanzibar kati yao watatu wakiwa na majeraha. Miongoni mwao wamo wazungu ambao inaaminika walikuwa wanaenda visiwani humo kwa shughuli za utalii.

Dkt. Mwadini alisema taarifa za kuzama kwa meli hiyo zilitolewa na Manahodha wa meli ya Mv Kilimanjaro, jana saa 7.50 mchana baada ya kuiona imepinduka na mgongo ukiwa juu.

Alisema meli hiyo ambayo ilibeba abiria na mizigo, inakisiwa ilibeba abiria wasiopungua 200 hadi 250 ambapo boti tano za uokoaji zilikwenda eneo la tukio, tatu kati ya hizo za watu binafsi na mbili za Serikali.

Aliongeza kuwa, waokoaji wanatoka Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM), Zima Moto, KVZ,  Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na polisi.

“Eneo maalumu limetengwa kwa ajili ya kupokea na kutambua maiti waliokufa katika ajali hii ambalo ni Viwanja vya Masaila ambavyo vilikuwa vikitumika kwa shughuli ya aina hiyo wakati wa tukio la kuzama kwa meli ya Mv Spice Islanders, iliyozama kwenye mkondo wa Nungwi, ikitoka Unguja kwenda Pemba.

Taarifa za kuzama kwa meli hizo ziliibua simanzi kubwa miongoni mwa wakazi wa Zanzibar, ambapo Jeshi la Polisi likilazimika kufunga Barabara ya Malindi inayoenda bandarini ambapo magari yakiyoruhusiwa kutumia barabara hiyo ni ya vikosi vya uokoaji.

Msemaji wa Jeshi wa Polisi Zanzibar, Bw. Mohamed Mhina alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, ingawa hakuwa na taarifa za kina wakati akizungumza na gazeti.

Mamlaka ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), nayo imethibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Ofisa Habari wa SUMATRA, Bw. David Mziray, alisema bado walikuwa wakiendelea kukusanya taarifa na baada ya kukamilika, watatoa maelezo kamili.

Watu walioshuhudia meli hiyo ikiondoka bandarini Dar es Salaam, walisema ilikuwa imejaza watu wengi kuliko uwezo wale. Mmoja wa mashuhuda hao, Bw. Abubakari Sadiki, alisema meli hiyo haina uwezo wa kubeba watu wengi kiasi hicho.

“Meli hii, inatakiwa kubeba watu 250 lakini leo (jana), iliondoka na watu wengi zaidi ya hao,” alisema Bw. Sadiki.

Tukio la kuzama kwa meli hiyo, limetonesha kidonda cha wananchi kwa kuwakumbusha lile la meli ya Mv Spice Islenders.


1 comment:

  1. ZANZIBAR IMEKATAA SUMATRA ISIFANYE KAZI ZANZIBAR SASA MAUAJI YA WASAFIRI KILA SIKU NA WATALII NAO WANAATHIRIKA WANATUHUMIWA KWA KURUHUSU MELI YA IRANI ITUMIEE BENDERA YA TANZANIA SHIDA NI KUTAKA KUONEKANA WANAWEZA KILA KITU SI VIBAYA ANDAENI RASILIMALIWATU POLEPOLE KABLA HAMJAJITENGA SINA UHAKIKA SERIKALI YA MUUNGANO IMEWATENGA ILA TUMECHOKA KULIA NA KUTOA RAMBIRAMBI NA KUMSINGIZIA MUNGU KATOA MUNGU KATWAA UONGO TU HATA JUMUIYA YA KIMATAIFA BAADAYE ITATUPUUZA WATALII WATATUKIMBIA TUNAOMBA IKIWEZEKANA LIWE TUKIO LA MWISHO HIVI WAZIRI ANAYESHUGHULIKA NA WIZARA HIYO NI VEMA ATANGAZE KUJIUZULU BILA HIVYO NI FREE-MASON ANAMASILAHI NA DAMU INAYOMWAGIKA

    ReplyDelete