20 July 2012
Nne zatinga nusu fainali Kombe la Stakishari
Na Heri Shaaban
TIMU nne zimefuzu kuingia nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Stakishari Ukonga wilayani Ilala kwa ajili maandalizi ya michuano ya Polisi Jamii Mkoa wa Ilala wa Kipolisi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkuu wa Polisi Wilaya Ukonga Stakishari ya Kipolisi, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Pili Mande alisema mashindano hayo yalianza Julai 16 mwaka huu ambayo yalishirikisha timu za Kata sita.
Pili alizitaja timu zilizoingia nusu fainali hiyo kuwa ni Kitunda, Segerea, Stakishari na Chanika ambapo mashindano hayo yalikuwa ya mtoano.
Alisema lengo la mashindano hayo ni kuimarisha ulinzi shirikishi, kujenga undugu na urafiki katika maeneo ya Wilaya Ukonga ya Kipolisi pamoja na kuunda vikundi vya ulinzi.
"Mashindano haya yameweza kuunda vikundi vya ulinzi jamii, sambamba na kuwapa mafunzo ya ulinzi wachezaji wa timu zote nane zilizoshiriki," alisema.
Alisema mechi za nusu fainali ya mashindano hayo, zinatarajia kufanyika Jumapili katika viwanja vya Stakishari Ukonga na wananchi wote wa eneo hilo wanaombwa kujitokeza kuangalia fainali hiyo.
Alitaja zawadi za washindi katika mashindano hayo, mshindi wa kwanza atajinyakulia kombe, mpira mmoja na seti moja ya jezi, wa pili atapewa seti moja ya jezi na mpira mmoja na wa tatu ataondoka na jezi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment