09 July 2012

Mbinu za kutokomeza ufisadi zabainishwa



Na Charles Mwakipesile, Mbeya

VIONGOZI nchini wametakiwa kutenda haki, kuwa na uzalendo ikiwemo kuacha ubinafsi kwa jamii ili kutokomeza ufisadi unalitikisa taifa.

Pia wametakiwa kuwa mfano wa miongoni mwa viongozi wachache wenye uchungu na uzalendo kwa nchi akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dkt. Charles Kimei kwa kumudu ambaye amekuwa mstari wa mbele kuchangia katika shughuli za maendeleo.


Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri, Dayosisi ya Kusini Njombe Bw. Isaya Mengele wakati akiongoza ibada ya harambee ya kuchangia Chuo Kikuu Kishiriki cha Tumaini kinachotarajiwa kuanzishwa katika kanda hiyo.

Alisema, viongozi wengi wakiwemo mawaziri na wabunge wamekuwa wakipigiwa kelele za ufisadi na wananchi waliowapa dhamana na kwamba wameshindwa kuwa wazalendo hivyo kuwafanya wananchi kukosa imani nao.

"Japo hawajathibitishwa, lakini kelele za wananchi kuhusu viongozi kughubikwa na ubinafsi na kukosa uzalendo wa nchi yao limekuwa likiongezeka kila wakati...lakini tuna baadhi ya viongozi wachache wenye uadilifu ambao wana uchungu na uzalendo na nchi yao kwa kutoa ajira kwa mamia ya Watanzania akiwemo Dk. Kimei," alisema Askofu huyo.

"Mtu anapoitwa fisadi hata kama hakuna ushahidi ina maana anakuwa anakwenda kinyume na maadili yaliyo mema...kwa miaka mingi Dkt. Kimei amekuwa akiongoza taasisi hiyo ya kifedha hapa nchini, lakini haijawahi kutokea kukutwa na kashfa yoyote na imekuwa miongoni mwa taasisi zinazotoa mchango mkubwa kwa nyanja zote za jamii," aliongeza.

Alisema, mchango wa Benki ya CRDB ni mkubwa kwa jamii nzima hata kanisa linatambua na kwamba inastahili kupata nishani ya heshima chini ya usimamizi wa Dkt. Kimei.

Akizungumzia kuhusu kumtolea Mungu, alisema moyo wa kumtolea mungu ni kibali kilichotolewa kwa kila mtu na kwamba haina maana kuwa matajiri peke yao ndiyo wenye mamlaka bali kila mtu ana jukumu la kutoa kile alichonacho na kitahesabiwa.

Akifungua harambee hiyo, Dkt. Kimei alisema benki yake imepata changamoto ya kuchangia jamii ikiwemo chuo hicho kitarajiwa kutokana na wadau wakubwa wa benki yake ni Watanzania wote bila kujali itikadi.

Alisema, kitakapoanzishwa chuo hicho kitasaidiwa kupunguza gharama, mrundikano wa wanafunzi kwenye vyuo vingine pamoja na umbali kupata huduma hiyo.

"Vyuo hivi ni muhimu kuanzishwa kwenye kanda hii kwa sababu itasaidia kuondoa mrundikano kwenye vyuo vingine, kupunguza gharama kwa walezi na wazazi wa kanda hii kutokana na hali ngumu ya maisha kwa sasa... pia kukaa karibu na familia vijana wengi watasoma kwa usalama zaidi, nidhamu itaongezeka na kuwaepusha na vitendo visivyofaa," alisema Dkt. Kimei.

Dkt. Kimei alisema kuwepo kwa vyuo vikuu kunachangia maendeleo katika jamii husika kutokana na kuongezeka kwa huduma mbalimbali ikiwemo za kibiahara na za kibenki.

"Benki yangu inachangia sh. milioni 50 na itashirikiana bega kwa bega katika maendeleo ya ujenzi wa chuo hiki kikuu kitarajiwa," alisema Dkt. Kimei.

Naye Mkuu wa Chuo Cha Ualimu Makumira Dkt. Gwamaka Mwankenja alisema mpango mkakati wa ujenzi na uanzishwaji wa chuo hicho zinahitajika sh. bilioni 33.6 ili kukamilisha mradi huo.

Alisema, katika kipindi cha mwaka 2012/2013 zinahitajika kukusanywa sh. bilioni mbili ambapo hadi sasa wamefanikiwa kukusanya michango mbalimbali kutoka kwa washarika na wadau sh. milioni 209,231,870.

Katika harambee hiyo, Dkt. Kimei alifanikiwa kukusanya sh. milioni 120 kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo zilizotolewa na benki yake.

No comments:

Post a Comment