09 July 2012

Wanunua madaraka CCM wasichekewe



MWAKA huu, Chama Cha Mapinduzi (CCM), kimeanza mchakato wa chaguzi mbalimbali ndani ya chama hicho na jumuiya zake.

Kimsingi chaguzi hizo zinapewa umuhimu mkubwa na wachambuzi wa masuala ya siasa na kuchukuliwa kama sehemu ya maandalizi ya chama hicho kushika dola katika Uchaguzi Mkuu 2015.


Ili chama hicho kipate viongozi bora wenye dhamira ya kutumikia wananchi ni vyema kikazingatia ushauri wa Rais Jakaya Kikwete aliosema, Serikali yake haipo tayari kuona uongozi unanunuliwa kama njugu ama shati.

Rais Kikwete aliyasema hayo mwaka 2011, mjini Mwanza wakati akifungua Mkutano Mkuu wa mwaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Alisema rushwa katika uchaguzi ni tatizo kubwa kama hatua za dhati hazitachukuliwa kwani kutoa na kupokea rushwa, inaonekana ni utaratibu wa kawaida.

Hivi sasa, vuguvugu la uchaguzi ndani ya CCM limeanza kushika kasi huku makada wakipigana vikumbo kuwania nafasi mbalimbali.

Sisi tunasema kuwa, kama wanachama CCM watazingatia kauli ya Rais Kikwete, wataweza kubadili mitazamo ya baadhi ya wanasiasa ambao kwa kiasi kikubwa, wameathiriwa na utaratibu wa takrima ambao umepigwa marufuku.

Kimsingi wanasiasa bado wana jukumu kubwa kuhakikisha wanaichukia rushwa kutoka ndani ya nafsi zao bila shinikizo la mtu au chombo chochote.

Imani yetu ni kwamba, rushwa ndani ya uchaguzi inachangiwa na wanasiasa matajiri baadhi yao ni wafanyabiashara ambao siasa kwao ni zaidi ya uongozi.

Rushwa inakwamisha maendeleo ya waananchi ambapo kama tutachagua viongozi wenye uwezo na sifa zinazostahili bila kutoa rushwa, watawajibika kutatua kero za wananchi.

Tukichagua viongozi makini, hawatatumia madaraka tuliyowapa kujinufaisha. Rushwa inakusa maadili yaliyooza, mambo muhimu katika maisha ni ukweli, sheria na utu.

Hayo ndiyo maadili makuu katika jumuiya yoyote hivyo umefika wakati, wanunua madaraka CCM kamwe wasichekewe.

No comments:

Post a Comment