30 July 2012
Matonya:Msanii wa bongo fleva aliyegeukia biashara *Ajenga hoteli ya Kifahari Tanga
Na Victor Mkumbo
NYOTA wa muziki wa kizazi kipya, Seif Shaban 'Matonya', ni mmoja wa wasanii wachache wenye mafanikio ambayo kwa njia moja au nyingine ni mfano wa kuigwa kwa wengine walioko kwenye tasnia hiyo.
Kumekuwa na wasanii mbalimbali ambao wanapata umaarufu mkubwa, lakini hawana maendeleo.
Hilo sio la kupinga kwani kuna wasanii wengi na wakongwe ambao walifanya vizuri katika tasnia hiyo katika miaka ya nyuma na sasa wapo tunawaona mtaani hawana mwelekeo.
Matonya sio jina geni hasa kwa wadau wa sanaa ya muziki wa kizazi kipya ambaye ameshafanya kazi hiyo kwa muda mrefu.
Msanii huyo alianza kuimba muziki wa kizazi kipya baada ya kujiona ana kipaji ambapo baadae alirekodi wimbo mmoja uliomtambulisha rasmi katika sanaa ya muziki.
Baada ya wimbo huo baada ya kumtambulisha rasmi alianza kushirikishwa katika nyimbo mbalimbali na baadhi ya wasanii na baadaye akaamua kuanza kuimba mwenyewe.
Matonya, anasema mafaniko yake yametokana na kujituma katika kazi na kusikiliza ushauri anapewa na wadau mbalimbali wa muziki huo, hali inayofanya kuwa kioo kwa wasanii wengine.
Anasema kupitia muziki, amefanikiwa kupata mafanikio mengi ikiwemo kutembea na kufanya muziki katika nchi mbalimbali za Ulaya, Afrika na kusaidia kumtangaza vema.
"Licha ya kupata mafanikio ambayo kwa sasa ninayo, nimepitia changamoto nyingi, lakini nashukuru mama yangu amekuwa msaada mkubwa katika kufikia mafaniko haya.
"Mara nyingi amekuwa akinishauri mambo mengi ambayo yananifanya kuwa katika mstari mnyoofu kwenye shughuli zangu za muziki, licha ya changamoto zinazojitokeza," alisema Matonya.
Baadhi ya mafanikio machache ambayo Matonya anajivunia kwa sasa ni kujenga hoteli ya kisasa iliyopo eneo la White Rose, Tanga.
Anasema hoteli hiyo iko katika hatua za mwisho kukamilika, hali ambayo inampa faraja kufikia hatua hiyo ambayo itamuweka katika sehemu nyingine ya mafanikio.
Licha ya kuwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, pia ni mfanyabishara wa magari, ambayo yamemsaidia kuendesha maisha yake, na ndiyo sababu kubwa iliyomfanya kuwa kimya kwa kipindi kirefu bila ya kuachia wimbo wowote.
"Biashara ya magari imenifanya kujiweka sawa katika maisha yangu, lakini zote zimetokana na kujihusisha na muziki, ambao ndiyo chimbuko lake, Pia, imetokana na kuupenda na kuuheshimu muziki wangu," anasema Matonya.
Anasema hoteli hiyo inatarajiwa kumgharimu sh. milioni 150, ambayo itafunguliwa hivi karibuni na itakuwa ni sehemu ya kutimiza ndoto zake katika maisha.
Licha ya kuwa na hoteli hiyo, lakini pia kupitia muziki na biashara zake, amefanikiwa kumiliki gari mbili za kifahari pamoja na nyumba moja Dar es Salaam, akiwa na nyumba mbili mkoani Tanga.
Msanii huyo, anasema baada ya mwaka huu kuisha na Mungu akimpa uhai, atakuwa Matonya mwingine kutokana na mafanikio ambayo atakuwa nayo kwa wakati huo.
"Nimejipanga vizuri kuhakikisha napata mafanikio makubwa mwakani kutokana na mambo mengi ambayo nayashughulikia kwa sasa kwenye biashara na kazi zangu za muziki," anasema Matonya.
Nyota huyo alianza kujiingiza katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya 2000, na baada ya miaka 10 amefanikiwa kuwa na mafanikio makubwa kwenye tasnia hiyo. Hakika ni jambo la kujivunia kwa upande wake.
Pia, msanii huyo anasema hakuna mtu ambaye anamtungia nyimbo kama baadhi ya wasanii wanavyojinasibu kupitia umaarufu alionao katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini.
"Nyimbo natunga mwenyewe na hakuna anaenitungia mashahiri na ndiyo maana nimefika pazuri katika mafanikio kupitia muziki kutokana na ubunifu mkubwa kwenye kazi hiyo," anasema Matonya.
Msanii huyo alianza kutambulika vema kwenye tasnia hiyo baada ya kuachia wimbo wa Vailet, ambao ulimuweka pazuri katika tasnia hiyo, ambayo sasa ana mafanikio ambayo ni mfano wa kuigwa.
Baada ya kutoka na kibao hicho, pia alichia vibao lukuki kikiwemo kinachofanya vizuri kwenye vituo mbalimbali vya redio na luninga cha Ajali Kazini pamoja na Mapenzi Kamari.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment