30 July 2012

'Mikataba mizuri ya kazi itamaliza migogoro kazini'



Na Gift Mongi

APRIL 23, mwaka huu kampuni ya sukari ya TPC iliyopo wilayani Moshi
mkoani Kilimanjaro, itatimiza miaka miwili tangu iliposaini mkataba wa
hali bora za wafanyakazi na chama cha wafanyakazi wa huduma za jamii
Tanzania (TASIWU), ikiwa ni hatua kubwa ya kumaliza mgogoro wa wafanyakazi uliodumu kwa zaidi ya miaka sita kiwandani hapo.


Mkataba huu ulisainiwa na pande hizo mbili mbele ya mkuu wa wilaya ya
Moshi Bw.Musa Samizi, ambaye pamoja na mambo mengine alitoa wito kwa
wafanyakazi wa TPC, kufungua ukurasa mpya baada ya kupata kile walichokihitaji kwa muda mrefu.

Makubaliano haya yalifikiwa baada ya kuwa na majadiliano kati ya pande
hizo mbili yaliyodumu kwa takribani siku 18, kupitia vipengele vya
mkataba huo na kujadili namna chama hicho kipya kipenzi cha wafanyakazi wa TPC, kitakavyoendesha shughuli zake na kuimarisha hali ya amani miongoni mwa wafanyakazi.

Chama hicho kipya ambacho kilikuwa miongoni mwa vyama ambavyo havikuunga mkono mgomo wa wafanyakazi uliokuwa ukihubiriwa na shirikisho la vyama vya wafanyakazi nchini (TUCTA), kinafanya jumla ya vyama viwili vinavyohudumia wafanyakazi wa TPC, kingine kikiwa ni kile cha TPAWU.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa TPC Bw.Robert Baisaac, raia wa Mouritius, anasema
makubaliano hayo ni hatua kubwa katika historia ya kiwanda hicho,
baada ya kukumbwa na migogoro, ambapo licha ya viongozi wa kada mbali
mbali kujaribu kuitatua hakukuweza kupatikana suluhu kwa kipindi chote
hicho.

Anasema kwa sasa kampuni hiyo inafungua ukurasa mpya kwa kushirikiana na vyama vyote viwili, kutekeleza matakwa ya mkataba huo, wa hali bora za wafayakazi, lengo kubwa likiwa ni kurejesha mahusiano yaliyopotea na pia kuongeza uzalishaji wa sukari kiwandani hapo.

TPC ilibinafsishwa mnamo mwaka 2000, kwa Mwekezaji M/S Sukari Investment Co. Ltd, ya nchini Mauritius ambaye anamiliki asilimia 75 ya hisa zote wakati serikali ikimiliki asilimia 25 ya hisa za kiwanda hicho.

Wakati kiwanda kinabinafsishwa na baadaye kutambuliwa kama kampuni ya
sukari ya TPC, kilikuwa kikizalisha wastani wa tani 34,892 na mipango
iliyokuwa imewekwa ililenga kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 72,
000 hadi kufikia mwaka 2005, kwa msimu mmoja, katika shamba lenye
ukubwa wa hekta 16,000 kati ya hizo hekta 7,800 zikiwa zinalimwa miwa
baada ya upanuzi uliofanywa mwaka
2005/2006.

Akizungumzia hatua hizo Ofisa Mtendaji Mkuu Baisaac, anasema sasa
umefika wakati wa kuongeza uzalishaji hadi kuvuka lengo hilo, na tayari wameweka lengo la kuzalisa hadi tani 85, 000 kwa msimu wa mwaka
2010/2011.

Msimu wa mwaka 2008/2009 kiwanda kilivunja rekodi ya uzalishaji kwa
kuvuna tani 787,000 za miwa ambazo zilifanikisha kutengeneza tani
78,400 za sukari, ambapo tangu kianze uzalishaji wake mwaka 2000,kimeilipa serikali kodi yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 40.

Hata hivyo wakati wa kusaini mkataba huo ameweka wazi kuwa mafanikio
hayo yatafikiwa endapo kutakuwa na mshikamano wa kweli, unaolenga
kuzalisha kwa wingi, hatimaye kuwezesha kampuni kuwalipa wafanyakazi
mishahara minono.

Bw.Jaffari Ally ni Ofisa Mtendaji Utawala, ambaye ni mmoja wa watu
waliokumbwa na mikasa mbali mbali wakati wa mgogoro kati ya wafanyakazi na uongozi wa TPC, na kupelekea kujeruhiwa kwa jiwe usoni
wakati wa mgomo ambao baadaye ulibainika kuhusisha vyama vya
wafanyakazi vya TPAWU na TUICO.

Alisema kwa muda wote huo wa mgogoro kiwanda kilipata misukosuko mingi
kiwemo kuzima mitambo yake hivyo kusimamisha uzalishaji wa sukari.

Hatua hii ilifikiwa baada ya wafanyakazi takribani 607, kushiriki kwenye mgomo wa Januari 23 na 24, mwaka 2007, na kuleta hasara ya dola 1,750,000 za Marekani baada ya kulazimika kufunga kiwanda hicho kwa siku saba mfululizo.

Januari 25 mwaka 2007 ndipo kiwanda kilisimamisha uzalishaji wa sukari
nakusababisha kupatikana hasara hiyo, kutokana na hatua iliyofikiwa na
wafanyakazi waliogoma ambapo wengine walidaiwa kuwashawishi wafanyakazi
ambao hawakuwa katika mgomo huo wajiunge kwenye mgomo.

Bw.Jaffari anasema licha ya migomo hiyo kesi mbali mbali zilizofunguliwa
na wafanyakazi waliosimamishwa kazi kwa kubainika kushiriki mgomo huo,
wapatao 168, ni sababu nyingine iliyochelewesha kufikia mkataba wa
hiari kati yapande hizo mbili.

Lakini anasema TPC, haikusita kukubali ombi la wafanyakazi kuchagua chama chao walichokitaka kuwawakilisha, bali kilichofanyika ni kufuata taratibu zote zilizowekwa kisheria.

Hata hivyo anasema licha ya kuwepo hali hiyo ya mvutano uongozi wa kampuni uliamua kuingia mkataba wa awali wa kukitambua chama kipya cha TASIWU, na baadaye kukaa kwenye meza ya majadiliano kuujadili mkataba huo ambao umesainiwa.

Alisema hatua hiyo inaonyesha utashi wa kampuni hiyo, katika kujali
maslahi ya wafanyakazi wake, na ndio sababu TPC, inakuwa mwajiri wa
kwanza kuwa na vyama viwili vya wafanyakazi kwa mkoa wa Kilimanjaro.

Ujio wa TASIWU, unaelezwa kuwa ukombozi mkubwa kwa wafanyakazi
kiwandani hapo, kwani tayari katika hatua za awali chama hicho katika
tawi lake la TPC, kimeweza kuwa na wanachama 1,892, kati ya wafanyakazi takribani 2000 wa kiwandani hapo.

Katibu Mkuu wa TASIWU Taifa, Bw.Christopher Nakuhwa, ameunga mkono hatua zote zilizofikiwa na uongozi wa kampuni hiyo, kuruhusu chama hicho
kuwa na tawi, kwani imelenga kurejesha mshikamano wa wafanyakazi, na pia kuweza kuelekeza jitihada zao katika uzalishaji wa sukari.

Bw. Nakuhwa anasema kazi kubwa ya chama chake ni kutetea maslahi ya
wanachama wake kwa mujibu wa katiba ya chama hicho na makualiano yaliyofikiwa kwenye mikataba hiyo, ili kuimarisha mahusiano sehemu ya
kazi.

Anasema katika kufikia malengo hayo, TASIWU, imeunda idara maalum ya huduma
kwa wanachama, ambayo itasikiliza malalamiko yote dhidi ya mwajiri,
hatimaye kuweza kuyatafutia ufumbuzi, lakini kwa mtazamo wa kuepukana
na migogoro.

Hata hivyo ameweka wazi kwamba hivi sasa migogoro mingi ya wafanyakazi
katika sehemu za kazi inasababishwa na misuguano ambayo imeanza kujitokeza miongoni mwa vyama vya wafanyakazi nchini, kwa sabau za
kimaslahi.

Katibu Mkuu huyo, anabainisha ukweli huo, wakati ambapo TPC, ikiwa ni moja
ya kampuni zilizokumbwa na mgogoro mkubwa wa wafanyakazi uliosababishwa na mvutano wa kimaslahi kwa vyama vya wafanyakazi vya TPAWU na TUICO.

Juni 2007, serikali ilibainisha kuwa mgogoro huo ulisababishwa na mvutano kati ya chama cha wafanyakazi wa mashambani (TPAWU) na kile
cha wafanyakazi wa viwandani na taasisi za fedha (TUICO).

Aliyekuwa Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana Bw.John Chiligati,
aliweka wazi kuwa vyama hivyo ndio vilikuwa chimbuko la mgogoro na
baadaye vyama hivi vilikutanishwa ambapo chama cha TUICO, kilitangaza
kutojihusisha kuwahudumia wafanyakazi kiwandani hapo.

Kwa kutambua uwepo wa vyama viwili vinavyohudumia wafanyakazi kiwandani hapo Katibu Mkuu wa TASIWU, Bw.Nakuhwa, anasema msingi mkubwa
wa kuepuka mgogoro wa vyama ni kufuata makubaliano yaliyofikiwa kwenye mikatba hiyo, na kujali
matakwa ya wafanyakazi ambao ndio wanachama wa chama hicho.

Lakini Katibu wa TASIWU Kanda ya Kaskazini Bw.Omary Nakuhwa
anatahadharisha ukiukwaji mkubwa wa sheria za kazi unaofanywa na vyama
vya wafanyakazi na kuwa chanzo cha migogoro sehemu za kazi.

Alisema hali hiyo inaibua malumbano yasiyokuwa ya msingi, hivyo kuondoa
maana nzima ya kuwa na vyama vya wafanyakazi, na badala yake kuvifanya
vionekane vyama vya kisiasa.

Hivyo ametaka mamlaka husika akiwemo msajili wa vyama vya wafanyakazi
nchi kutambua dosari hizo ili kufanyia marekebisho hayo ambayo
yameanza kuleta athari kubwa sehemu mbali mbali za kazi kutokana na
ukiukwaji huo wa sheria za kazi unaofanywa na baadhi ya vyama vya
wafanyakazi nchini.

Hii ni hatua kubwa na muhimu katika kutatua migogoro sehemu za kazi,
baada ya kuwepo baadhi ya vyama vya wafanyakazi vilivyotambua umuhimu
wa kuzifuata sheria za kazi, na kutambua madhumuni ya kuanzishwa kwake
katika mchakato mzima wa kuwa na majadiliano kati yake na waajiri
nchini.

TPC ni miongoni mwa viwanda vinne vya kuzalisha sukari hapa nchini,
vingine ni Kilombero, Mtibwa na Kagerakati hivyo viwanda vya Mtibwa
na Kilombero,hutegemea miwa inayolimwa na wakulima wa nje.

No comments:

Post a Comment