17 July 2012
Mataifa zaidi ya Afrika yajiunga APRM
Na Mwandishi Wetu, Addis Ababa
MATAIFA zaidi ya Afrika, yamesaini mkataba wa kujiunga na mchakato wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), wakati wa kikao cha Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika (AU), zinazoshiriki katika tathmini ya APRM mjini hapa.
Mkutano wa huo umefanyika mwishoni mwa wiki ambapo Rais Jakaya Kikwete, aliongoza marais wa Afrika ambao walihudhuria mkutano huo ambapo nchi hizo ni Niger, Cape Verde na Chad.
Nyingine ni Tunisia na Guinea ya Ikweta, hivyo kufikisha idadi ya nchi 36 kati ya 54, ambazo ni wanachama wa AU walioamua kujiunga na mchakato wa APRM.
Kwa mujibu wa Ofisa Habari na Mawasiliano wa APRM Tanzania, Bw. Hassan Abbas, alisema APRM huipa nchi fursa ya kuanzisha taasisi yake ya ndani ili kuwapa wananchi nafasi ya kuitathmini nchi yao katika utawala bora.
“Tathmini hii huakikiwa na wataalamu wengine kutoka nchi za Afrika na kila nchi kujikosoa ili baadaye kujisahihisha,” alisema.
Akizungumza baada ya mkutano huo, Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania, Bi. RehemaTwalib, alisema viongozi hao walipitisha maazimio mengi likiwemo kuiimarisha APRM ili kuwa taasisi kamili ya Umoja wa Afrika.
Rais Kikwete aliunganana marais wengine akiwemo Bw. Jacob Zuma wa Afrika Kusini, Waziri Mkuu wa Ethiopia, Bw. Melesi Zenawi na Rais wa Uganda, Bw. Yoweri Museveni.
Mkutano huo pamoja namambo mengine pia ulijadili taarifa ya utekeleza wa hali ya utawala bora kwa nchi za Uganda, Burkina Faso na Algeria ambapo Rais Abdulaziz Bouteflika wa Algeria aliwakilishwa na Waziri Mkuu, Bw. Ahmed Ouyahia.
Tanzania ni miongoni mwa nchi za Afrika ambazo zimejiunga na mpango huo tangu uanzishwe mwaka 2003 kwa kusaini mkataba mwaka 2004 na Bunge likauridhia mwaka 2005.
Tayari ripoti iliyosheheni maoni ya Watanzania kuhusu utawala bora nchini imeshakamilika.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment