09 July 2012

Makamba aanika mikakati ya kuiendeleza Bumbuli



Na Mwandishi Wetu

MBUNGE wa Bumbuli, mkoani Tanga, Bw. January Makamba, amesema jimbo hilo limejipanga kufanya mageuzi ya kuongeza pato la wakulima kutokana na mazao wanayolima kwa kuboresha mbinu za kilimo na kuhifadhi mazao yao.

Bw. Makamba ambaye ni Mwenyekiti wa mageuzi hayo kupitia mpango Maalumu, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akiainisha mikakati hiyo kwa waandishi wa habari.

Alisema lengo la mpango huo mbali ya kuchochea maendeleo pia utavutia wawekezaji ambao watajenga taasisi au shule ambazo walimu, wanafunzi na wafanyakazi wake watatumia bidhaa zinazozalishwa jimboni humo.

“Hatua hii itasaidia kutengeneza ajira na fursa za kujiongezea kipato kwa wananchi, mpango huu pia utasaidia kuanzishwa taasisi ya fedha ambayo hatimaye itakuwa Benki ya Wananchi wa Jimbo la Bunguli na kutoa mikopo yenye masharti nafuu,” alisema.

Aliongeza kuwa, wanakusudia kuchukua hatua za kuhifadhi mazingira ya Milima ya Usambara kwani maisha na maendeleo ya wakazi wa Bunguli kiuchumi, hutegemea mandhari ya mlima huo.

“Tuna mpango wa kuanzisha Shirika la Maendeleo Bumbuli ambalo litakuwa na jukumu la kubuni, kuratibu na kusimamia uendeshaji wa shughuli mbalimbali na litakuwa kiini cha mtandao wa kijamii,” alisema Bw. Makamba na kuongeza kuwa, lengo la kuanzisha shirika hilo ni kuchochea maendeleo ya jimbo si vinginevyo.

Bw. Kamaba alisema, shirika hilo limesajiliwa kama kampuni yenye ukomo wa dhamana na litafanya biashara ili kulipia gharama za uendeshaji na faida ambayo itapatikana, itatumika kugharamia miradi ya maendeleo ili kufikia malengo ya kijamii ya Mkakati wa Mageuzi ya Kiuchumi jimboni humo.

1 comment:

  1. Nijambo la furaha sana kuona kuwa Mbunge wetu wa Bumbuli kuwa na maono haya mazuri kipekee nikiwa mwana Bumbuli,namuomba Mbunge wetu atengeneze mazingira yakuweza kukutna na wana Bumbuli wa hapa Dsm hata na mikoa mingine maana hayo ni maendeleo yetu wenyewe pamoja na Taifa,namtakia heri ya mafanikio ya malengo hayo na mungu aibariki kazi ya mikono yake. Amen. Rebecca

    ReplyDelete