09 July 2012

Lukindo: Utatuzi migogoro ya ardhi Handeni unahitaji busara ya viongozi


Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya watu watano iliyoundwa na wakazi wa Mkoa wa Tanga kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wananchi katika sekta ya kilimo cha zao la mkonge, maji, elimu na ardhi, imesema sakala la migogoro ya ardhi wilayani Handeni, linahitaji busara ya viongozi waliopewa dhamana ya uongozi na Rais Jakaya Kikwete.


Akizungumza na Majira Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Abraham Lukindo, alisema upo umuhimu mkubwa wa Serikali kuwachunguza Maofisa Ardhi wilayani humo ili kubaini kero mbalimbali zilizosababisha na idara hizo.

Alisema pamoja na Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Muhingo Rweyemamu kutoa siku 14 kwa watu wanaomiliki ardhi hekta 16,000 kujisalimisha kwake, chanzo cha migogoro mingi ya ardhi wilayani humo imetokana na viongozi wenye dhamana serikalini.

“Bw. Rweyemamu ametoa siku 14 kwa vigogo wa Serikali na watu binafsi wanaomiliki hekta hizi kujisalimisha kwake, ukweli ni kwamba, historia ya migogoro ya ardhi Handeni ni kubwa.

“Wapo Maofisa Ardhi ambao wamehusika kutengeneza hati bandia na kuuza ardhi kinyume na taratibu, umefika wakati wa kuunda tume ambao itahusika kuwachunguza maofisa hawa, watendaji na madiwani ambao wamehusika kutengeneza hati bandia.

“Viongozi wa Serikali wametumia nguvu kubwa kupora maeneo na kuwapa ndugu zao pamoja na marafiki ushahidi huo tunao,  namuomba ndugu yangu Bw. Rweyemamu, atekeleza jukumu alilonalo bila kutugawa na kusababisha migogoro zaidi,” alisema.

Aliongeza kuwa, dhamana ya Bw. Rweyemamu ni kubwa wakiamini kuwa, kila mkazi wa Handeni ni mtoto wake wakiwemo vichaa, wezi, waumini wa dini zote, wazee pamoja na watoto kama mwakilishi wa Rais Kikwete.

 kuongoza wananchi utatuzi wa migogoro mshukuru Mbunge wa Handeni, mkoani humo, Dkt. Abdallah Kigoda kwa kuridhia kuonana na ujumbe huo.

Alisema pamoja na siku 14 alizotoa kwa watu wanaomiliki ardhi kujisalimisha kwake, wahusika wanapaswa kutafakari agizo lipi walifuate la Mkuu wa Wilaya, Rais Kikwete au Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

“Rais amewaomba Wakuu wa Wilaya wasiingilie maamuzi ya Mahakama ambapo Julai 6 mwaka huu, Profesa Tibaijuka akiwa bungeni mjini Dodoma, alisema mtu akivamia shamba lako hakikisha unampeleka polisi, nani mwenye kauli ya mwisho.

“Je, tufute kesi zote zilizopo mahakamani na kuzihamishia ofisini kwa Mkuu wa Wilaya, ndio maana tukasema busara inahitajika zaidi kutatua migogoro iliyopo,” alisema Bw. Lukindo.

Bw. Lukindo alimshukuru Mbunge wa Jjimbo hilo, Dkt. Abdallah Kigoda ambaye pia ni Waziri wa Viwanda na Biashara kwa kukubali kukutana na kamati hiyo ili kujadili kwa pamoja changamoto mbalimbali zinazowakabili wakazi wa mkoa huo.

No comments:

Post a Comment