23 July 2012

Madiwani wapinga agizo la serikali


Na Suleiman Abeid, Kishapu

KATIKA hali isiyo ya kawaida, madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, wamepinga vikali agizo la Serikali ambalo limewataka kupunguza ushuru unaotozwa kwa wanunuzi wa zao la pamba kutoka asilimia tano hadi mbili.


Madiwani hao wametoa msimamo huo juzi baada ya Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Bw. Lucas Said, kuwasomea barua kutoka kwa Katibu Tawala wa Mkoa (RAS), yenye kumbukumbu namba CA.64/253,01B/33.

Barua hiyo ya Julai 11 mwaka huu, alikuwa ikiagiza kufanyika kwa  mabadiliko ya viwango vya ushuru.

Wakionesha kukerwa na agizo hilo, madiwani hao walisema kaama kiwango hicho cha ushuru kitapunguzwa ni wazi halmashauri hiyo itapoteza sh. milioni 720 hivyo kuathiri mipango yao ya maendeleowaliyonayo kwa wananchi.

Walisema mwaka 2011, halmashauri hiyo ilipata hati chafu ya ukaguzi wa hesabu zake hivyo haiwezi kupatiwa fedha za ruzuku kutoka Serikali Kuu kwa ajili ya shughuli za maendeleo.

Waliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo ni wazi kwamba shughuli zote za maendeleo mwaka 2012/13 utekelezwaji wake utatokana na mapato ya ndani pekee hivyo kitendo cha kuteremsha kiwango cha ushuru kitawaathiri wakazi wa Wilaya hiyo pamoja na wakulima.

“Hatupo tayari kushusha ushuru huo ambao tayari umepitishwa na kuingizwa ndani ya bajeti ya mipango ya maendeleo, tunaiomba Serikali itafute njia mbadala ya kumfidia mkulima badala ya kuzilazimisha halmashauri kuharibu bajeti zao kwa ajili ya kurekebisha bei ya pamba kwa mkulima,” alisema.

Madiwani hao walidai kusikitishwa kwao na tabia ya Serikali kuingilia mapato ya halmashauri hiyo na kulazimisha kufuta sheria ndogo inazojitungia ili kujiongezea mapato yake.

Walisema inasititisha halmashauri kuzuiwa wasilipwe mapato yoyote kutoka mgodi wa almasi Mwadui na kuchukua mapato yanayotokana na mnada wa Mhunze.

No comments:

Post a Comment