16 July 2012

Madaktari nchi nzima kuandamana *Lengo ni kupinga dhuluma, uonevu dhidi yao



Rehema Maigala na Stella Aron

CHAMA cha Madakatari Tanzania (MAT), kimetangaza kufanya maandamano ya amani jijini Dar es Salaam ambayo yatajumuisha madaktari kutoka mikoa mbalimbali nchini ili kufikisha kilio chao kwa Serikali.

Madaktari hao, leo wameandaa mkutano wa dharura uliolenga kujadili mwenendo wa taaluma hiyo nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Katibu wa MAT, Dkt. Rodrick Kabangila, alisema maandamano hayo yamepangwa kufanyika wiki ijayo na yataanzia katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) hadi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.

Maandamano hayo yatashirikisha wanaharakati, taasisi za kutetea haki za binadamu na wananchi mbalimbali ambapo madaktari wote watavaa makoti yao meupe na wasio madakatari watavaa vitambaa vyeupe.

“Tunawaomba wananchi wote wenye mapenzi mema na taaluma ya udaktari, wajitokeze kushiriki maandamano haya ili kufikisha kilio chetu serikalini,” alisema Dkt. Kabangila.

Aliongeza kuwa, Serikali imesitisha usajili wa zaidi ya madakatari 400 walio chini ya usimamizi, walio kazini na bado wameendelea kufanya hivyo wakati daktari mmoja nchini, anahudumia wagonjwa 30,000.

Dkt. Kabangila alisema, MAT inasikitishwa na dhuluma ambayo inaendelea kufanywa na Serikali dhidi ya taaluma ya udaktari na madaktari wenyewe hivyo inapanga kufanya mabadiliko ya baadhi ya vikwazo vinavyochangia taaluma hiyo kupokwa haki zao.

“Lengo la maandamano haya ni kupinga dhuluma na uonevu ambao unaoendelea dhidi ya taaluma ya udaktari na madaktari wenyewe, tunalaani kitendo alichofanyiwa Dkt. Steven Ulimboka cha kutekwa, kupigwa, kuteswa na kutupwa katika msitu wa Mabwepande.

“Tunataka Serikali iunde tume huru kuchunguza suala hili haraka ili wahusika wakifikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema.

Wakati huo huo, mwakilishi wa madaktari walio kwenye mafunzo ya vitendo, Dkt. Frank Kagalo, alisema orodha iliyotolewa na Serikali kwa kusitisha usajili wao, baadhi yao wapo likizo ya kawaida, uzazi na wengine walishamaliza mafunzo muda mrefu.

Alisema kitendo cha Serikali kusitisha usajili wa madaktari hao si njia ya kutatua mgogoro huo kwani tayari baadhi ya madaktari wameamua kwenda kufanyakazi nje ya nchi.

Aliongeza kuwa, wapo baadhi ya madaktari ambao wameamua kuandika barua za kuacha kazi kwa hiari yao wenyewe na wengine wameamua kuachana kabisa na fani hiyo.

“Usitishwaji wa usajili, si njia ya kumaliza mgogoro hivyo wapo baadhi ya madaktari ambao wameamua kwenda nje ya nchi, pia wapo madaktari bingwa ambao wanatarajia kuandika barua za kuacha kazi muda wowote,” alisema.

Alisema uamuzi ulitolewa na Serikali wa kusitisha usajili wa madaktari hao, haukizingatia sheria kwani umesikiliza upande mmoja na Baraza la Madaktari la Tanganyika, bado lina kasoro nyingi ambapo Mwenyekiti wake ndiye Mganga Mkuu wa Serikali.

“Mfumo wa hili baraza unahitajika kubadilishwa, kwanza lipo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, madaktari walio kwenye mafunzo kwa vitendo wanafanyakazi chini ya usimamizi wa daktati bingwa lakini baraza hilo halikuangalia usawa wa suala hilo,” alisema Dkt. Kagalo.

Alisema madaktari wa interns, hawakufika kazini kwa sababu ya ukosefu wa madaktari bingwa hivyo hawawezi kufanya kazi bila usimamizi wa madaktari hao.

“Daktari bingwa hawapo kazini, sisi hatuwezi kufanyakazi bila wao kwani kufanya hivyo, kunaweza kuhatarisha maisha ya wagonjwa tangu madaktari wapewe barua, mgogoro huu ndio umezidi kukua badala ya kupungua,” alisema.

Hata hivyo, Dkt. Kagalo alisema ni hatari kubwa kama Serikali itaamua kuwachukua madaktari kutoka kwenye zahanati na kwenda kufanyakazi kwenye Hospitali za Rufaa.


No comments:

Post a Comment