16 July 2012
Bei ya pamba yapingwa kwa mapanga Shy
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
KATIKA hali isiyo ya kawaida, wakulima wa zao la pamba Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, jana wamefanya vurugu kubwa na kuzuia wanunuzi kutonunua zao hilo sh. 660 kwa kilo moja.
Hali hiyo inatokana na wakulima hao kupinga bei iliyotangazwa na Bodi ya Pamba (TCB), wiki iliyopita wakidai hairejeshi gharama walizopata kwenye kilimo cha zao hilo.
Akizunghumza na Majira, mmoja wa wakulima wa zao hilo (jina tunalo), alisema jana wakulima waliweka vizuizi barabarani kuzuia magari yote ya wanunuzi wa pamba yaliyokuwa yakienda vijijini.
Alisema eneo ambalo limeathirika zaidi kutokana na vurugu hizo ni Jimbo la Bariadi Mashariki, ambalo lipo chini ya mbunge Bw. John Cheyo (UDP), ambako baadhi ya wakulima walikuwa na silaha za jadi kuzuia watu ambao watajaribu kununua pamba kutoka kwa wakulima kwa bei ya sh. 660.
“Ni kweli kama mlivyosikia, huku kwetu kuna vurugu kubwa, watu wamefunga barabara, wakulima wamegoma kuuza pamba yao kwa bei ya sh. 660 kwa kilo moja.
“Pia wametishia kupambana na mtu yeyote ambaye ataonekana kununua pamba kwa bei hii, wamedai kuuza zao hilo kwa bei iliyotangazwa na Serikali itasababisha wapate hasara,” alisema.
Baadhi wa wakulima wameiomba Serikali iangalie uwezekano wa kuwalipa fidia kama ilivyofanya kwa wanunuzi wa zao hilo mwaka 2010 walipodai uchumi wa dunia uliyumba na kuhoji kwanini iweze kuwafidia wanunuzi na kushindwa kufanya hivyo kwa wakulima.
“Ipo hatari ya watu kuumizana, tukio hili la leo (jana), linaonesha wazi kwamba hivi sasa wananchi wamechoka kwa kutotendewa haki na kuamua kujichukulia sheria mkononi katika suala ambalo Serikali imeshindwa kulipatia ufumbuzi wa uhakika hasa masilahi yao ya kila siku,” alisema mkulima huyo.
Mkazi wa Bariadi mjini, Bi. Monica Kayangosi, alisema vurugu hizo zimesababisha baadhi ya mabasi ya abiria kupita kwa shida na kuhatarisha usalama wa abiria.
Habari zilizotufikia wakati tukienda mtamboni zinadai kuwa, mkulima mmoja ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Nyamalapa, jana mchana alishambuliwa na wakulima wenzake wakati akijaribu kuuza zao hilo kwa bei ya sh. 660.
Inadaiwa kuwa, nyumba ya mkulima huyo pia imechomwa moto ambapo Jeshi la Polisi mkoani hapa, limethibitisha kutokea kwa tukio hilo. Hadi jana jioni, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa ilikuwa ikiendelea na kikao ili kutoa taarifa rasmi
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment