02 July 2012

Lushoto yawaweka sawa wakandarasi wanaolaumu



Na Yusuph Mussa,Tanga

BAADHI ya wakandarasi wilayani Lushoto wamelalamika kuwa hawapewi kazi wilayani humo kwa madai hawana vigezo ikiwemo ukarabati wa barabara na kudai kazi hizo wanapewa wakandarasi kutoka Kanda ya Ziwa, kutokana na urafiki na baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki kwa kuomba majina yao kutoandikwa gazetini wakandarasi hao, walimtupia lawama Mhandisi wa Ujenzi Wilaya ya Lushoto Bw. Stanley Mgaya kwa kusema anawapa kazi wakandarasi aliokuwa anafanya nao Manispaa ya Musoma mkoani Mara.

"Mkandarasi alieondoka, pamoja na kuwa alikuwa na kampuni yake, lakini alikuwa anaturushia mifupa (baadhi ya kazi), lakini sio huyu wa sasa, yeye anachukua wakandarasi kule alikokuwa anafanya kazi mkoani Mara," alisema mmoja wakandarasi hao ambaye aliomba jina lake kutoandikwa gazetini.

Mkandarasi mwingine, alisema hawana imani na Bodi ya Zabuni ya Wilaya ya Lushoto, kwani imeonesha kuwakandamiza wakandarasi wazawa wa wilaya hiyo na kuwapandelea wageni hivyo kuwafanya walipe kodi Mamlaka ya Mapato (TRA) bila kufanya kazi.

Hata hivyo Mhandisi wa wilaya Bw. Stanley Mgaya alipoulizwa kuhusu shutuma hizo alisema, sio kweli bali wakandarasi wa Lushoto walizoea kufanya kazi kwa mazoea lakini kutokana na kazi za sasa kutangazwa kwenye magazeti wanaomba watu kutoka maeneo mbalimbali.

"Kwanza sio kweli wakandarasi wa Lushoto hawapati kazi, barabara nyingi, majengo ya shule na zahanati wanapewa wakandarasi wazawa, sema wao wanafanya kazi kwa mazoea. Wanashindwa kuelewa sasa hivi kazi zinatangazwa nchi nzima kupitia magazeti, hivyo mtu yeyote kutoka Tabora, Mwanza au Mara anaweza kuomba," alisema Bw. Mgaya.

Katibu wa Zabuni Wilaya ya Lushoto Bw. Deogratius Lyampawe alikanusha kuwakandamiza wakandarasi wazawa kwa kusema wanashindwa kufikia vigezo, huku akisema ushindani wa kazi umeongezeka kutokana na kazi kutangazwa magazetini.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Bw. Lucas Shemndolwa alisema hajapokea malalamiko yeyote ofisini kwake yanayoonesha wakandarasi wa wilaya hiyo wananyimwa kazi huku akitahadharisha wao hawawezi kushinikiza wapewe kazi.

"Sijapata malalamiko hayo, lakini nafasi yetu kama madiwani sio kushinikiza nani apewe kazi, ila kazi yetu ni kusimamia uteuzi wa wakandarasi uwe umezingatia kanuni na taratibu. Kama kuna uteuzi ambao haukusimamia haki, mlalamikaji anatakiwa kutoa lalamiko lake kwa ngazi husika.

"Yapo makampuni ya wazawa ambayo yanafanya kazi. Mwezi huu nimesaini mkataba wa Kampuni ya Mwanafunyo inayotengeneza Barabara ya Mlola- Makanya- Milingano na nyingine Africa One Barabara ya Dochi hadi Mombo," alisema Bw. Shemndolwa.

No comments:

Post a Comment