02 July 2012
Zatakiwa kushughulikia vipigo kwa wanawake
Na Godfrida Jola
SERIKALI za vijiji, wilaya na mikoa zimetakiwa kushughulikia suala la vipigo kwa wanawake ili kupunguza vifo kwao wakati wa kujifungua.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Kitaifa (DHS), kwa mwaka 2010 katika kila wanawake 100,000 wanaojifungua umebainisha kuwa wanawake 454 hupoteza maisha.
"Vipigo vimekuwa kama janga la kitaifa, wanawake wanapigwa sana na kubaki na vilema vya kudumu na wengine mimba zinaharibika huku takwimu kamili zikifichwa katika madawati ya kushughulikia masuala hayo, katika madawati ya jinsia na polisi wilayani;
Hayo yalisemwa jana Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waaandishi wa Habari Wanawake nchini (TAMWA) Bi.Ananilea Nkya wakati akitoa ripoti ya utafiti uliofanywa katika mikoa 20 nchini ikiwemo
mitano ya Zanzibar kuhusu hali ya vitendo vya ukatili nchini.
Utafiti huo ulioshirikisha vyombo mbalimbali vya habari na TAMWA, ulibaini kuwa, baadhi ya viongozi katika ngazi ya wilaya hawatoi ushirikiano kwa wanahabari wanaoandika habari za kuhamasisha maendeleo
nchini ikiwemo vijiji vya Tarime, Mvomero, Kinondoni, Temeke, Njombe na Kondoa.
Viongozi wengine hawapatikani ofisini ili kuweza kutoa ushirikiano kwa wanakijiji au wanahabari wanaofika katika ofisi hizo kupata takwimu na taarifa za maendeleo ikiwemo Kijiji cha Bicha kilichopo Wilaya ya
Kondoa Mkoa wa Dodoma na Kijiji cha Bolisa Kata ya Bolisa.
"Tunaiomba serikali iweke utaratibu kwa kurekodi taarifa na takwimu mbalimbali za ukatili wa kijinsia ili wanahabari wapate kirahisi, viongozi wa wilaya na vijiji wanatakiwa kuwapa wanahabari ushirikiano kama rafiki zao ili kupunguza vitendo hivyo;
"Tunawaomba shule na ofisi za vijiji ziweke takwimu kuhusiana na mimba shuleni ili kujua ni watoto wangapi wanakatisha masomo na kuwasaidia kulitatua tatizo hilo," alisema Bi.Nkya.
Vitendo vilivyolegwa katika utafiti huo ni ubakaji, vipigo kwa wanawake, kutelekeza watoto na wanawake, ukeketaji pamoja na kulazimisha watoto wa kike kukatisha masomo ili waolewe.
*****************
Polisi wamshikilia
mwanake na madawa
Na Mary Margwe, Manyara
MKAZI mmoja wa mtaa wa Songambele Mji Mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, Bi. Martha Kirika (46) anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara akidaiwa kukamatwa na madawa ya kulevya aina ya bangi, mirungi na pombe haramu ya gongo.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo jana, Kamanda wa Polisi mkoani hapa Bw. Akili Mpwapwa alisema tukio hilo lilitoke Mtaa wa Songambele mji mdogo wa Mirerani.
Kamanda Mpwapwa alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na misokoto 92 ya bangi na mabunda 25 ya mirungi ikiwemo lita moja ya pombe haramu ya moshi maarufu kama gongo.
Alisema, mwanamke huyo alikamatwa juzi kwenye msako maalum wa kupambana na uhalifu na kuimarisha doria ulioongozwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Mirerani Mrakibu Msaidizi Ally Mkalipa, Mkaguzi Naftal Mnzava na Sajini Joseph Mirambo.
Alisema kuwa, jeshi lake linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo na pindi upelelezi huo utakapokamilika wanatarajia kumfikisha mahakamani mtuhumiwa huyo kwa shauri hilo.
“Zoezi hili ni endelevu na linaendelea sehemu zote za mkoa wetu, ili kuhakikisha kuwa vitendo vya uhalifu vinapungua kama si kwisha kabisa na ninawapongeza vijana wangu kwa kulifanikisha zoezi hili la kupambana na uhalifu katika mkoa huu,” alisema Kamanda Mpwapwa.
Kamanda Mpwapwa alitoa mwito kwa wakazi wa mkoa huo wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu kuacha mara moja kwani jeshi lake limejipanga vizuri kupambana na uhalifu wa aina yoyote ile na kuwachukulia hatua kali wale watakaobainika kuhusika na tukio lolote la uhalifu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment