19 July 2012

Korogwe yageuka uwanja wa vita *Maiti zaburuzwa na kamba barabarani, wanne wapigwa risasi



Na Yusuph Mussa, Korogwe

MAUAJI ya kutisha jana yametokea mjini Korogwe, mkoani Tanga baada ya wananchi kuwachoma moto watu wawili wanaodaiwa kumuua mwenyesha pikipiki ya kubeba abiria maarufu 'bodaboda, Bw. Athuman Ramadhan (28) yaliyotokea Julai 13 mwaka huu, katika Kijiji cha Kwamzindawa, Kata ya Mnyuzi.


Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa, Kamanda wa Polisi mkoani Tanga, Constantine Masawe, alisema waliouawa na kuchomwa moto hawajajulikana majina yao, lakini ni watu wenye umri kati ya miaka 25 hadi 35 na maiti zao zimehifadhiwa Hospitali ya Magunga mjini Korogwe.

Alisema tukio hilo limetokea saa nne asubuhi kwenye eneo la Mountain View mjini Korogwe, ambapo vijana wa bodaboda walipata taarifa kuwa watuhumiwa wanaodaiwa kumuua mwenzao wapo eneo hilo hivyo waliwazingira lakini polisi walifika mapema.

“Baada ya polisi kufika eneo hilo ili kuwachukua watuhumiwa, bado walishindwa kutokana na wingi wa wananchi, pamoja na askari kupiga risasi za moto hewani na kupiga mabomu ya machozi, hawakukimbia na kuzuia watu hao wasiondolewe.

“Kutokana na hali hiyo, polisi walilazimika kupiga risasi kwenye kundi la wananchi ambao wanne ziliwapata sehemu mbalimbali ambao ni Bw. Shaban Omar (25), risasi ya kifua, Bw. Akili Mussa (40), Bw. Kobelo Mloka (24), walipigwa miguuni na Bw. Tawfiq Kuziwa (18), dereva wa bodaboda, pajani,” alisema.

Kamanda Masawe alisema askari waliojeruhiwa katika mapambano hayo ni Sajent Raphael na PC Sikujua ambapo hadi jana jioni, hakuna mtu aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.

Mwandishi alishuhudia waendesha pikipiki wakiziburuza maiti hizo barabarani baada ya kuzifunga kamba zaidi ya kilomita tatu na kwenda kuzichoma moto katika Uwanja wa Chuo cha Ualimu Korogwe, huku wananchi wakishangilia.

Sababu nyingine iliyofanya polisi wazidiwe nguvu ni kutokana na Mkuu wa Wilaya hiyo, Bw. Mrisho Gambo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya na askari zaidi ya 50, tangu juzi walikuwa Kijiji cha Kwenkeyu, Kata ya Kizara, ambako walikwenda kukamata wananchi wanaolima bangi.

Akizungumza na Majira, polisi mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe gazetini kwa sababu si msemaji alisema kuwa, waendesha bodaboda wilayani humo walishatoa taarifa polisi kuwa wakiwapata wauaji wa mwenzao, mapambano yatakuwa kati ya polisi na wao, kwani hawatakubali waokolewe lazima nao wauawe.

2 comments:

  1. KINACHOSIKITISHA NI KITUO CHA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA KIMEGEUKA CHAMA CHA SIASA CHA UPINZANI KIMESHINDWA KABISA KULAANI MATUKIO HAYA NI KAMA KIMEBARIKI WATU WAUANE TU HII SUMU ISIPOKEMEWA IKISAMBAA TUSUBIRI SYRIA NYINGINE TANZANIA HII NI MARA YA PILI TUMESHUHUDIA MTUHUMIWA WA WIZI WA PIKIPIKI AKICHOMWA BAADA YA KUVALISHWA TAIRI HUYU ALIONEKANA KAMA KUKU TU WALA HALIKURIPOTIWA WALA KULAANIWA JANA ILIKUWA WACHOMWE WATATU WAWILI WALICHOMWA YULE WA TATU ALIZUIWA NA POLISI KWA RISASI ZA MOTO TUNAMSHUKURU MBUNGE WA KOROGWE VIJIJINI MAARUFU MAJIMAREFU KUFIKA NA KUWAPUNGUZIA MUNKARI TUNAOMBA HATUA ZA DHATI ZICHUKULIWE AMA SIVYO KIZAZI CHA KESHO KITAFIKIRI HIYO NDIO NJA MUAFAKA YA KUPAMANA NA UHALIFU WATAKUWA KAMA ISRAEL NA PALESTINA

    ReplyDelete
  2. NI KWELI HAINA UBISHI KUNA USIASA KATIKA KUTEKELEZA MAJUKUMU YA KITUO CHA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA KUUA WATUHUMIWA NA KUWABURUZA WATU BARABARANI KILOMETA BARABARANI NI MATESO MAKALI KULIKO KULIKO YALE YA DR.ULIMBOKA LAKINI PICHA ZA MAREHEMU HAO HAZIKUWEKWA WALIVYOKUWA WANABURUZWA HATA WABUNGE SI LOLOTE SI CHOCHOTE SIJAONA MBUNGE KULAUMU KITUO HIKI LICHA YA RAIS WAKATI FULANI KUONYESHA MASHAKA JUU YA UTENDAJI WAKE HIVI UCHUNGUZI UKIONYESHA HAWANA HATIA KAMA MTUHUMIWA ALIYETUHUMIWA KULIPUA NDEGE YA LOCABEE JE KITUO KIKO TAYARI KUSHITAKIWA KWENYE MAHAKAMA YA KIMATIFA?????

    ReplyDelete