19 July 2012
Kamishna Uhamiaji Zanzibar alipuliwa bungeni
Na Benedict Kaguo, Dodoma
MBUNGE wa Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Bw Haji Khatib Kai (CUF), amemlipua bungeni Kamishna wa Fedha na Utawala, Idara ya Uhamiaji Makao Makuu, Bw. Peniel Mgonja
kuruhusu kutolewe hati mbili za kusafiria kwa raia wawili wa Rwanda kinyume na sheria za nchi.
Bw. Kai amelipua bomu hilo wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na kuongezsa kuwa, kwa mujibu wa sheria za nchi, hairuhusiwi raia wa kigeni kupewa hati ya kusafiria isipokuwa katika Taifa lake jambo ambalo kwa makusudi kiongozi huyo aliruhusu lifanyike.
Alisema Bw. Mgonja alikuwa na watu wake wawili raia wa Rwanda ambao walikuwa wakitaka hati za kusafiria na kumpa kazi hiyo mtumishi wa idara hiyo ili ashughulikie suala hilo lakini baada ya kuwahoji, aligundua sio raia wa Tanzania bali waanatoka Twanda.
“Hawa watu walikuwa hawjui vizuri Kiswahili lakini Bw. Mgonja alimtaka Ofisa huyu wa Uhamiaji ahakikishe watu hao wanapatiwa hati za kusafiria.
“Baadae Ofisa wa Uhamiaji alisema ni vigumu kuwapa hati za kusafiria kwa sababu si raia hivyo Bw. Mgonja, alidai kumuonesha mtumishi huyo kuwa yeye ni nani,” alisema Bw. Kai.
Aliongeza kuwa, Ofisa huyo kwa kutambua majukumu yake na kutii sheria za nchi, alikataa kutoa hati hizo kutokana na sheria kutoruhusu watu hao kupewa hati hizo.
“Kamishna huyu alipoona Ofisa wake amekataa kuvunja sheria, alimwambia atampa adhabu ya kumpeleka Mtambaswala ambapo hivi sasa amehamishwa hayupo tena Makao Makuu,” alisema.
Akizungumza na Majira nje ya ukumbi wa Bunge, Bw. Kai alisema taarifa alizonazo, Ofisa huyo amehamishiwa Dar es Salaam na kupelekwa Loliondo kwa ajili ya kukagua wageni wanaokwenda kunywa dawa 'kikombe cha babu'.
Alisema ushahidi wa tuhuma zote anao akitakiwa kuthibitisha atafanya hivyo pamoja na kulalamikia mfumo wa kuleana ambao unaendelea katika idara hiyo na kuhoji nani anawapa kiburi watumishi kama hao.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Ukerewe, mkoani Mwanza, Bw. Salvatory Machemli (CHADEMA), alisema wananchi wa visiwa vya Ukerewe wamekosa imani na Jeshi la Polisi.
Alisema hali hiyo inatokana na jeshi hilo kushindwa kudhibiti matukio ya mauji na uporaji ambayo yanaendelea visiwani humo.
“Mauji ya watu 15 yaliyokuwa yametokea katika visiwa hivi, yalihusishwa na askari polisi wa Kituo cha Nansio ambaye hivi amehamishwa badala ya kuchukuliwa hatua,” alisema.
Aliongeza kuwa, silaha za kivita na bundiki za SMG zilitumika kupora katika kwenye tukio lililotokea Julai 15 ambalo nalo limehusishwa na polisi ambao wamekuwa wakitumia silaha kuwaangamiza wananchi.
“Mheshimiwa Spika, tangu tuvamiwe na kutaka kuuawa kwa kupigwa mapanga hadi sasa, sijawahi kuitwa kuhojiwa...walau niwataje niliowaona siku hiyo lakini polisi wameishia kuhoji upande mmoja, leo tunaambiwa kesi iko Mahakamani huku ni kutunyima haki ya kuhojiwa,” alisema Bw. Machemli.
Alisema msimamo wake ni kwamba, polisi wanashirikiana na makundi ya wahalifu hasa katika Ziwa Victoria.
Mbunge wa Maswa Mashariki, Bw. Sylvester Kasulumbayi (CHADEMA), alisema kama polisi wote watapewa likizo kwa saa mbili, Taifa litashudia mauji ya kutisha.
Alisema Polisi ni watu muhimu lakini Serikali kwa muda mrefu imekuwa ikiwatelekeza na kushindwa kuwawekea mazingira mazuri ambapo hali ya majengo ya askari katika Wilaya hiyo ni mbaya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment