10 July 2012

Kituo cha kumbukumbu kuanzishwa Amboni



Na Anneth Kagenda

KITUO kikubwa cha kumbukumbu na taarifa kwa ajili ya vivutio vidogo vya utalii nchini kinatarajiwa kujengwa eneo la Amboni mkoani Tanga.

Hayo walisemwa na Mkuu wa Sehemu ya Uenezi na Mawasiliano Idara ya Mambo ya Kale  Bw. Mwita Williamu wakati akizungumza na gazeti hili katika maonesho ya Kimataifa ya 36 ya Biashara yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere Sabasaba Dar es Salaam.


Bw. William alisema kuwa kituo hicho ambacho kitawanufaisha wakazi wa mkoa huo na Watanzania kwa ujumla mchoro wake tayari umekamilika na kilichobaki ni kuanza ujenzi.

"Lengo letu ni kuhakikisha tunaleta huduma nzuri na za haraka kwa wananchi, lakini pia katika kivutio cha Amboni tumeweza kufanya mabadiliko makubwa kwani hivi sasa kuna umeme pamoja na tochi kubwa za kuchaji ambazo zinatumika kuwashia ndani kwa watu wanaokuwa wakiingia ndani ya kivutio hicho kufanya utalii," alisema Bw. William.

Aidha alisema kuwa, kituo hicho kitakuwa kikitoa taarifa mbalimbali kuhusu maeneo mengine yaliyopo nchini.

Kwa upande wake Msemaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bw. George Matiko alisema kuwa, mara baada ya kituo hicho kujengwa kitatoa fursa mzuri ya watu kujua taarifa ambazo zipo kwenye vivutio vingine ambavyo kwa wakati huo watakuwa hawajaviona.

"Lakini tofauti na suala hilo pia tunashukuru kwani tumepata ushindi wa kwanza wa lundi la wizara, wakala na Idara za Serikali zinazojitegemea baada ya kushindanishwa ambapo tumebahatika kupata kikombe na cheti," alisema Bw. Matiko.

Hata hivyo aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kwenda kuelimishwa juu ya wanavyotakiwa kushiriki katika utekelezaji wa sera ya maliasili nchini.

"Mwaka huu katika maonesho haya tunasisitiza utalii wa ndani nia yetu ikiwa ni kwamba wazawa wawe na kasumba ya kutembelea vivutio vya ndani," alisema.

No comments:

Post a Comment