10 July 2012

Moto wa Mwakyembe usizimwe



Na Stella Aron

UPANDAJI wa nauli kiholela umekuwa kikwazo kikubwa kwa abiria na kusababisha usumbufu na unaopelekea baadhi ya watu kushindwa kusafiri.

Mara nyingi malalamiko ya kupanda kwa nauli kwa mabasi yaendayo mikoani hufanyika katika vipindi tofauti huku wahusika wakiendelea kulifumbia macho suala hilo.

Kutokana na mfumuko wa bei unaosababisha ugumu wa maisha kwa wananchi wengi hali hiyo imekuwa kama ni kikwazo kwa wananchi wanaosafiri kwa kutumia mabasi.

Licha ya kuwepo kwa mamlaka husika bado suala la upandaji wa nauli kiholela limekuwa kero kwa abiria.

Katika kuhakikisha ukweli wa suala hilo, jana Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe aliamua kukitembelea Kituo Kikuu cha Mabasi yaendayo mikoani Ubungo ili kubaini ukweli huo.

Dkt. Mwakyembe ameamua kubaini kero za wananchi kwa kujionea mwenyewe ambapo tayari amejionea madudu katika usafiri wa reli ambao alitumia wakati akienda kwenye kikao cha Bunge kinachoendelea.

Katika safari hiyo Mwakyembe alibaini uchafu kutokana na kuwepo kwa ulanguzi wa tiketi na kuwataka wafanyakazi wa malaka ya reli kurekebisha kasoro hizo.

Jana Waziri Mwakyembe alijionea madudu mengine katika kituo cha mabasi ya mikoani ambapo alifika kituoni hapo alfajiri na kupanda kwenye mabasi tofauti huku akiuliza abiria mmoja mmoja kiasi alicholipa na kubaini hutofauti.

Kutokana na kitendo hicho, Dkt. Mwakyembe aliweza kubaini baadhi ya abiria kupandishiwa nauli na kulazimika kuyarudisha mabasi hayo na kisha kurudisha nauli walizoziongeza kwa abiria.

Kwa kitendo hicho ninampongeza Waziri Mwakyembe kwani sasa ameamua kufanyakazi kwa kufika kwenye matukio na si kusubiri taarifa aletewe ofisini.

Kutokana na moto huo aliouwasha ni bora waziri huyo akaendelea na juhudi hizo bila ya kuwekewa vikwazo mbalimbali.

Utendaji kazi wa namna hiyo ndio unaotakiwa kwani baadhi ya watendaji si waaminifu kwa kuweka maslahi yao mbele ya kupeleka taarifa kwa viongozi tofauti.

Nionavyo mimi ni kuwa, utendaji kazi wa Dkt. Mwakyembe unapaswa kupongezwa kwani ni viongozi wachache wenye kunyuka ofisini na kwenda kwenye matukio.

Kwa ufanyaji kazi wa namna hiyo nina imani kuwa ataweza kubadilisha kasoro mbalimbali zilizoko kwenye sekta yake.

Pia ni vizuri viongozi wengine wakaiga mfano wa waziri huyo na kwa kuendelea kufanya hivyo nina imani kuwa Taifa letu lenye amani litapunguza ubadhirifu na rushwa zinazotawala katika sekta mbalimbali.

Kiongozi mwajibikaji ni yule anayependa kushuhudia kinachoendelea kwa watendaji wake na si kusubiri ripoti kwenye makaratasi.

Tukifanya hivyo watendaji wetu wataweza kutimiza wajibu wao na hata kuondokana tabia ya kukaa ofisini pale tu wanaposikia watatembelewa na viongozi kutoka ngazi za juu.

Ni muda mrefu wananchi wamekuwa wakitaka viongozi wa namna hiyo ambao wanafika kwenye matukio na kujionea wenyewe ukweli na si kusoma kwenye magazeti na taarifa wanazopewa.

Nina imani kuendelea kwa moto huo kutaleta changamoto kwa viongozi wengine kuiga na hata kuweka mikakati inayoendana na sekta zao kwa kuzipatia ufumbuzi.

Tusimwachie Rais Jakaya Kikwete kwenda kuibua kero mbalimbali za wananchi ila ni wajibu wenu kumsaidia na kumpa taarifa za ukweli na uhakika na kumpa mwongozo wa kuzitatua.

Uwaziri si cheo pekee bali wanatakiwa kufanyakazi kwa vitendo zaidi ili kuonyesha uwezo ambao walipewa ambao hawakuomba wala kutarajia.

Viongozi wengi wanaofanya hivyo tunaona maendeleo yao kwani kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa kwani hakuna atakayevuruga utaratibu uliowekwa.

Msingi wa maendeleo ni mpango na kile unachokipanga kukifanya ukikisimamia inawezeka kikakutoa katika hatua uliyopo.

No comments:

Post a Comment