16 July 2012
Kesi ya EPA yazidi kupigwa tarehe
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana imeshindwa kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa wa kesi ya wizi wa sh. bilioni 5.9 za Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Washtakiwa katika kesi hiyo ni pamoja na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bw. Rajabu Maranda na wenzake kutokana na jopo la mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo kutokamilika.
Kesi hiyo inasikilizwa na jopo la mahakimu watatu ambao ni Bw. Ilvin Mugeta, Bw. Stuwart Sanga na Bi. Lita Tarimo.
Wakili wa Serikali Bw. Shadrack Kimaro, aliiambia mahakama hiyo kuwa kesi hiyo ilikuja ajili ya washtakiwa kuwasomea maelezo ya awali pamoja na kuunganishwa kwa mshtakiwa mwingine aliyemtaja kwa jina la Mwakyosa.
Hakimu Bi. Tarimo alisema kesi hiyo haiwezi kusikilizwa kutokana na mmoja wa mahakimu wanaosikiliza kesi hiyo, Bw. Mugeta, kuwa mjini Dodoma kwa majukumu mengine ya kikazi, hivyo aliiahirisha hadi Julai 26 mwaka huu.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Bw. Farijala Hussein, Bw. Ajay Somani na ndugu zake Bw. Jai Somani pamoja na wafanyakazi wawili wa BoT, Bi. Ester Komu aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Madeni na Bw. Bosco Kimela ambaye alikuwa Kaimu Katibu wa BoT.
Inadaiwa kuwa, washtakiwa hao kwa pamoja walikula njama na kutenda makosa hayo kati ya Desemba 2004 na Mei 2005, jijini Dar es Salaam.
Katika kesi hiyo, Bw. Maranda anadaiwa kughushi hati za uongo na kuziwasilisha Benki ya Baroda, akionesha kuwa Bw. Thabit Mapunda ni mwana hisa wa Kampuni ya Liquidity Services Limited.
Ilidaiwa kuwa, kati ya Septemba 2 na Desemba 13 mwaka 2005, Bw. Maranda, Bw. Somani na Bw. Jai walijipatia zaidi ya sh. bilioni 3.97 kutoka BoT baada ya kudanganya kuwa, Kampuni ya Liquidity, imepewa deni na Kampuni ya M/S Societe Alsacienne De Construction De Machines Textiles ya Ufaransa.
Alidai kati ya Septemba 2 na Desemba 13 mwaka 2005, Bw. Maranda alijipatia zaidi ya sh. bilioni 1.93, kutoka BoT, baada ya kudanganya kuwa, Kampuni ya Liquidity imepewa deni na Kampuni ya M/S Societe ya Ufaransa.
Aliongeza kuwa, Agosti 30, mwaka 2005, Bi. Komu na Bw. Kimela, wakiwa waajiriwa wa BoT, waliisababishia benki hiyo hasara ya sh. bilioni 5.9.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment