16 July 2012
CWT: Serikali ifanye mazungumzo na walimu kutatua mgogoro uliopo
Na Jovither Kaijage, Ukerewe
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), Wilaya ya Ukerewe, mkoani Mwanza, kimeitaka Serikali kutumia meza ya mazunguzo kutatua changamoto za walimu badala ya vitisho na vyombo vya dola kuzuia haki yao.
Katibu wa CWT wilayani hapa, Bw. John Kafimbi, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na Majira juu ya tetesi zilizopo kuwa Serikali imejipanga kutumia vitisho na vyombo vya dora kuzuia
mgomo wa walimu.
Alisema chama hicho kimefuata taratizo zote za kisheria kabla ya kuitisha mgomo wa walimu nchi nzima hivyo hawatarajii chombo chochote kitazuia mgomo huo kama muafaka hautapatikana kwa kukaa meza moja na Serikali.
Bw. Kafimbi ambaye ni Mjumbe wa Baraza Kuu la Taifa CWT, alisema zipo taarifa kuwa Serikali kwa kutumia Maoafisa Elimu ngazi za Wilaya na viongozi wengine wa ngazi za juu, wamepewa maelekezo ya kuwatisha walimu.
Amezitaja hatua ambazo Serikali imedhamiria kuzichukua kuwa ni pamoja na kuhakikisha Walimu Wakuu ambao ni viongozi wa CWT wananyang'anywa nyadhifa zao na kuwapa vitisho vya kuwafuta kazi hivyo wamejipanga kukabiliana navyo kisheria.
“Lengo la CWT ni kuakikisha tatizo lililopo linatatuliwa kwa njia ya mazungumzo ndio maana tumekubaliana na ombi lao la kutaka waongezewe muda hadi Julai 23 mwaka huu.
“Msimamo wa chama ni kuitisha mgomo kama Serikali itashindwa kutekeleza maombi yao na kutaka walimu wajiandae kwa mgomo wa kutoenda kazini,” alisema Bw. Kafimbi.
Aliwataka walimu nchini kupuuza taarifa zilizotolewa hivi karibuni na baadhi ya walimu wa Halmashauri ya Ujiji Kigoma badala yake watambua kuwa, Msemaji wa CWT ni Rais wa chama pekee.
Hivi karibuni baadhi ya walimu wa halmashauri hiyo waliwatuhumu viongozi wa CWT kwa madai ya kushindwa kutatua matatizo ya walimu na wamekuwa wakijinufaisha wao kwa kuanzisha vitega uchumi ambavyo faida yake haijulikani kwa walimu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment