23 July 2012

Kampeni ya kutangaza utalii wa Tanzania yazinduliwa Marekani



Na Mwandishi Maalumu, Marekani

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, juzi alishiriki uzinduzi wa kampeni maalumu ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini katika mji wa Seattle nchini Marekani.

Katika kampeni hiyo, Balozi Kagasheki alieleza matarajio yake ya kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea nchini kuangalia vivutio mbalimbali katika kipindi kifupi kijacho.


Kampeni hiyo, ilihusisha uwekaji mabango yanayotangaza vivutio vya utalii nchini katika mechi ya Mabingwa wa Ulaya, kati ya  Chelsea na Seattle Sounders.

Akizungumza katika kampeni hiyo, Balozi Kahasheki alisema Tanzania imekuwa ikiutumia mpira wa miguu kutangaza vivutio vyake katika maeneo mbalimbali nchini.

“Safari hii tumegeukia katika mji wa Seattle wenye wapenzi wengi wa soka ambao kutokana na maatangazo haya, wataweza kuvutiwa na kutembelea vivutio vya utalii nchini. Tanzania,” alisema.

Aliongeza kuwa, uzinduzi wa matangazo hayo yatawafikia watazamaji milioni 400 kwa mwaka kupitia televisheni ambazo zinarusha mechi mbalimbali na wale wanaofika katika uwanja wa Seattle Sounders.

Mji wa Seattle ni soko muhimu Magharibi mwa Marekani lenye wakazi wenye kipato kizuri na wanaotembelea maeneo mbalimbali duniani kwa ajili ya shughuli za utalii.

Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini Marekani Bi. Mwanaidi Maajar, alifurahishwa na kampeni hiyo na kusema kuwa, imekuja kwa wakati muafaka kwani mahitaji ya Wamarekani kutembelea vivutio vya utalii nchini yamekuwa yakiongezeka.

“Kampeni hii itasaidia kuongeza idadi ya wageni nchini na kufikia lengo la wageni milioni moja kwa mwaka kutoka laki nane waliopo sasa,” alisema Bi. Maajar.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi ya Utalii nchini, Dkt. Aloyce Nzuki, ambaye bodi yake inahusika na utangazaji wa vivutio vya utalii nchini, alisema kampeni hiyo ni moja ya mikakati madhubuti ya bodi yake kuhakikisha wanatumia mbinu mbalimbali kupenya katika masoko mapya ili kuvutia wageni.

“Lengo ni kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania  ili kujionea vivutio mbalimbali hivyo kuongeza pato la Taifa,” alisema.

Katika uzinduzi huo, Tanzania ilipata fursa ya kuwa na banda maalumu na kutoa maelezo juu ya vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa wageni mbalimbali waliofika kwa ajili ya kushuhudia mchezo wa Chelsea na Seattle Sounders pamoja na kugawa vipeperushi.

No comments:

Post a Comment