02 July 2012
Ilala yaingia mkataba na Green Waste Pro Ltd
Mwali Ibrahim na
Heri Shaban
HALMASHAURI ya manispaa ya Ilala imeingia mkataba wa miaka mitatu na kampuni ya usafi ya Green Waste Pro Ltd kwa ajili ya kufanya usafi katika baadhi ya maeneo ya Manispaa hiyo.
Kampuni hiyo itaanza usafi rasmi leo katika maeneo ya Kisutu, Kivukoni na Mchafukoge katika Manispaa ya Ilala.
Akizungumza Dar es Salaam jana, wakati wa kuzindua mkakati huo Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Bw. Said Meck Sadik alisema, wanaimani katika kipindi hicho usafi katika jiji hasa maeneo ya Ilala ambayo yamekuwa na sifa kubwa ya kuwa na uchafu yatakuwa katika hali nzuri.
Aliongeza kuwa, licha ya Halmashauri hiyo kuingia mkataba na kampuni hiyo lakini pia Watanzania wanatakiwa kutambua kuwa usafi ni jukumu la kila mtu hivyo kila mmoja ajitume katika kuhakikisha anayaweka mazingira safi kwa kuepuka kutupa takataka hivyo.
Lakini pia amesisitiza elimu ya usafi kwa wananchi ili iweze kuwasaidia zaidi katika kutambua majukumu yao katika mazingira.
Kwa upande wake Meya wa Manispaa ya Ilala Bw.Jerry Sila alisema, karibu mwaka mzima alikuwa akizungumzia mikakati ya usafi Ilala na sasa imefika mwisho ilichobaki sasa ni kazi tu.
Alisema mkakati huo unatarajia kuanza Julai Mosi mwaka huu na halmashauri imetenga shilingi milioni 90 kwa ajili ya kulipia fidia eneo la kituo
Naye Mkurugenzi wa kampuni hiyo Bw.Anthony Shayo alisema, kampuni yake imejipanga katika kuhakikisha maeneo hayo waliyopatiwa wanayafanyia usafi ipasavyo kutokana na kutumia vifaa vya kisasa zaidi.
"Tuna magari ya kufagia hadi kudeki katika maeneo yanayo staili, lakini pia tuna magari ya kuzolea taka kwa kiasi kikubwa huku taka zikiwa hazionekani ambapo zikishazolewa na kuingia katika gari kunamashine za kuzisaga na kuzidi kupungua hivyo kuweka taka nyingi," alisema.
Alisema, pia watatumia wafanyakazi wengine kufanya kazi kwa mikono katika maeneo ambapo magari hayawezi kupita huku wakitumia bajaji zao katika kukusanya uchafu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment