11 July 2012
Hukumu ya Prof. Mahalu kusomwa leo
Na Rehema Mohamed
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, leo inatarajiwa kutoa hukumu ya kesi ya uhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya sh. bilioni mbili.
Kesi hiyo inamkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia Profesa Costa Mahalu na Bi. Grace Martin, ambaye alikuwa Mkuu wa Fedha na Utawala katika ubalozi huo.
Hukumu hiyo inatarajiwa kutolewa mbele ya Hakimu Bw. Ilvin Mugeta, anayesikiliza kesi hiyo baada ya kumaliza kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili.
Juni 8 mwaka huu, upande wa utetezi ulifunga ushahidi wao baada ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, Bi. Martin kumaliza kujitetea.
Prof. Mahalu anatetewa na mawakili Bw. Mabere Marando, Bw. Beatus Malima, Bw. Alex Mgongolwa na Bw. Cuthbert Tenga. Miongoni mwa mashahidi waliokuja kumtetea ni pamoja na Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Bw. Benjamin Mkapa.
Katika hukumu hiyo, miongoni mwa hoja muhimu ambazo zitazingatiwa ni pamoja na Serikali ya Tanzania kama ilimruhusu Prof. Mahalu kununua jengo la ubalozi kwa njia ya mikataba miwili ambayo ni euro 3,098,741.58.
Nyingine ni kama muuzaji wa jengo hilo hakupokea fedha za manunuzi ambazo ni euro milioni tatu.
Washtakiwa walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza mwaka 2007 wakikabiliwa na mashtaka sita, ambayo ni kula njama kutenda kosa la wizi na kughushi vocha ya malipo ya ununuzi wa jengo.
Mengine ni kughushi mikataba miwili ya ununuzi wa jengo hilo kwa ajili ya kuidanganya Serikali, kutumia risiti ya ununuzi wa jengo hilo kuidanganya ili waioneshe kwa Serikali kuwa walimlipa muuzaji euro milioni moja wakati si kweli na kuisababishia Serikali hasara ya kiasi hicho cha fedha za kigeni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment