26 July 2012

Hukumu kesi ya Mtikila Agosti 27


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imepanga kutoa hukumu ya kesi ya kuchapisha na kusambaza waraka wa uchochezi dhidi ya Rais Jakaya Kikwete inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila Agosti 27 mwaka huu.


Hukumu hiyo itatolewa mbele ya Hakimu Bw.Ilvin Mugeta anayesikiliza kesi hiyo baada ya upande wa utetezi kufunga ushahidi wao.

Akifunga ushahidi huo,Mchungaji Mtikila alidai kuwa anafunga ushahidi wake kwa sababu hataki kupoteza fedha za Serikali kuleta maaskofu kutoka Mwanza kuja kumtetea kwa kuwa anaamini watakuja kuieleza mahakama kilekile alichokwisha kieleza yeye.

Hakimu Mugeta alimueleza Bw.Mtikila kuwa ni wazo zuri kutopoteza fedha za umma kwani jambo la msingi kuamini alichokieleza mahakamani.

Jana kesi hiyo ililetwa kwa ajili ya utetezi ambapo shahidi wa mwisho anayemtetea Bw.Mtikila alikuwa mwandishi wa habari wa Gazeti la Mwananchi Bw.Mpoki Bukuku.

Katika utetezi wake Bw.Bukuku alitoa kielelezo kimoja ambacho ni gazeti la Mwananchi la Agosti 6, 2009 lililokuwa na kichwa cha habari 'Mtikila apiga kampeni Kanisani kumpinga JK'
'Achunguzwa na Polisi kumwaga sumu Rais asichaguliwe 2010'.

Akitoa ushahidi wake Bw.Bukuku aliieleza mahakama hiyo kuwa habari hiyo ilikuwa ikiripoti kilichotokea Mwanza katika mkutano wa maaskofu lengo likiwa ni kuelimisha jamiii.

Alidai kuwa anaamini habari hiyo haikuwa na tatizo lolote kwa sababu polisi hawajalalamika kwani kama habari ikiwa na matatizo huomba radhi au hufanya mapatano mengine.

Aliongeza kuwa habari hiyo ilikuwa inahusu mafundisho ya viongozi wa dini.

Katika kesi hiyo Mtikila anadaiwa kuwa kati ya Januari 2009 na Aprili 17, 2010 jijini Dar es Salaam, kwa nia ya uchochezi, alisambaza kwa umma nyaraka zilizosomeka 'Kikwete kuuangamiza ukristo', 'wakristo waungane kuweka mtu Ikulu'

Mtikila alikiri kuandaa waraka huo na kusambaza nakala zaidi ya 100,000 nchini, huku akidai kuwa waraka huo si wa uchochezi bali unahusu maneno ya Mungu.

No comments:

Post a Comment