26 July 2012
ALAT yasikitishwa na ung'olewaji wa viongozi halmashauri
Na Mwandishi Wetu
JUMUIYA ya Tawala za Mitaa na Tanzania (ALAT),imesikitishwa na mtindo unaotumika kuwang'oa viongozi wa Halmashauri kwa kuwatuhumu kwa kutumia utaratibu ambao ni kinyume cha sheria.
Mwenyekiti wa ALAT Taifa, Dkt.Didas Masaburi alisema wamepokea taarifa za vurugu katika Halmashauri mbalimbali nchini hivyo ingependa kuona zinaendeshwa kwa kuzingatia utawala bora na utawala wa sheria na haki.
"Taratibu zinaeleleza kuwa endapo Halmashauri ya wilaya/miji itakuwa na sababu ya kutosha kumwondoa madarakani mwenyekiti wake, madiwani wasiopungua theluthi moja watamtumia Mkurugenzi wa Halmashauri ombi la maandishi lililotiwa saini zao wakimtaka aitishe mkutano wa dharura wa kuzungumzia kumwondoa madarakani mwenyekiti wao" alisema Bw, Masaburi.
Dkt.Masaburi ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam alisema ili hoja ya namna hiyo ikubalike ipelekwe kwenye kikao cha Halmashauri (Full Council) na iwe na tuhuma yenye ushahidi wa kutosha na kutolewa maelezo kamili na yenye kueleweka na tuhuma zinazohusika.
Aliwaasa viongozi hao waache vurugu kama wanazo tuhuma basi watumie utaratibu iliowekwa kwa mujibu wa sheria bila kufuata utaratibu huo vurugu zitatokea na halmashauri kushindwa kutekeleza wajibu wao wa kutoa huduma bora.
Alisema kutokana na vurugu hizo ALAT inatarajia kuitisha kikao cha Kamati ya Utendaji kujadili matukio yanayoendelea na hatimaye kuonana na waziri mwenye dhamana ya Serikali ya Mitaa ili kuondoa hayo yaliyojitokeza.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment