30 July 2012

Flying Eagles yaiduwaza Ngorongoro



Na Mwandishi Wetu

TIMU ya Taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka 20 ya Nigeria (Flying Eagles), imeishangaza timu ya Taifa ya Vijana ya Tanzania wenye umri huo (Ngorongoro Heroes) kwa kuichapa mabao 2-1.

Mchezo huo ulipigwa jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ukiwa na wa kwanza hatua ya pili ya kuwania kucheza fainali za 18 za Afrika.

Fainali za michuano hiyo imepangwa kufanyika mwakani nchini Algeria.

Katika mechi hiyo, timu zote ziliuanza mchezo kwa kasi huku kila moja ikifanya mashambulizi ya kushtukiza ambapo mpaka dakika 10 za kwanza zilikuwa hazijafungana.

Dakika ya 16, Achaji Gero alifunga bao la kwanza kutokana na mabeki wa Ngorongoro kufanya uzembe wa kushindwa kuokoa na mpira kumkuta mfungaji aliyekwamisha mpira wavuni.

Mchezaji huyo alionekana kuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Ngorongoro kwani dakika ya 42, aliifungia timu yake bao la pili akimalizia krosi iliyopigwa na Aminu Umar.

Ngorongoro katika kipindi hicho ilifanya shambulizi la nguvu dakika ya 32 kupitia kwa Atupele Green akiwa katika eneo la hatari alishindwa kukwamisha mpira wavuni kwa kupiga shuti lililotoka nje.

Timu hiyo dakika nne baadaye ilifanya tena shambulizi la nguvu kupitia kwa Ramadhani Singano ambaye alipiga shuti lililoookolewa na kipa Samuel Okani na mabeki kuondosha hatari.

Kipindi cha pili, Ngorongoro ilifanya mabadiliko kwa kumtoa Jamal Mroki na kuingia Hassan Kondo, badiliko lililozaa matunda ambapo dakika ya 49, Green alifunga bao la kwanza kwa kichwa akiunganisha krosi ya Singano.

Baada ya kufunga bao hilo, Ngorongoro ilikuja juu na kufanya mashambulizi ya nguvu katika dakika za 60 na 74 kupitia kwa Simon Msuva na Green ambapo washuti yao yalitoka nje na mengine kudakwa na kipa.

Mpaka dakika 90 zikimalizika, Flying Eagles iliibuka na ushindi wa mabao 2-1, hivyo kuipa wakati mgumu Ngorongoro katika mechi ya marudiano itakayochezwa jijini Lagos.

Wakati mechi hiyo ikiendelea, Kocha Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen alikuwa akisaidiana na kocha wa Ngorongoro, Jakob Michelsen kwenye Benchi la Ufundi kuhakikisha timu hiyo inaibuka na ushindi katika mechi hiyo.

Ngorongoro:Barwany Khomein, Omega Seme, Jamal Mroki/Hassan Kondo, Issa Rashid, Ruhana Samir, Yarouk Ramadhan, Kheri Salum/Jerome Lambele, Frank Domayo, Simon Msuva, Green na Sindano.

No comments:

Post a Comment