30 July 2012
100% tz Flava yakuna mashabiki wa burudani
Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro Lager, ni miongoni mwa kampuni ambazo hushirikiana na jamii katika mambo mbalimbali.
Ukiangalia kwa haraka bia hiyo, imekuwa ikiiweka jamii pamoja kupitia michezo kwa kuandaa tuzo za wanamuziki (Kili Music Awards) pamoja na udhamini kwa timu kongwe nchi za Simba na Yanga.
Miaka miwili iliyopita, bia hiyo katika kujiweka pamoja na jamii ilianza safari kwa kupeleka bendera yetu ya Taifa kukimbizwa kutoka Dar es Salaam mpaka kilele cha Mlima Kilimanjaro na kuifikisha bia hiyo katika kilele cha mafanikio.
Mwaka jana ilisherehekea miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania huku bia hiyo ndio bia pekee iliyokuwa na kila sababu ya kujivunia kuangalia tulipotoka na tunapokwenda kama Taifa.
Baada ya mambo hayo, sasa bia hiyo inaangalia ilipotoka na kufurahia inapokwenda kwa kusherehekea kilicho tofauti na mataifa mengine ulimwenguni kwa kuwapa wateja wake 100% tz Flava.
100% tz Flava ni promosheni ambayo ina lengo la kuelekeza mtizamo wao kwenye vitu halisi vya kibinafsi vinavyoelezea uTanzania halisi.
Kutokana na hali hiyo,ndio maana wakaanzisha kampeni hiyo ya kwanza ambayo inaelezea vitu vyote ambavyo vimezaliwa Tanzania na vikajengeka Kitanzania.
Miongoni mwa vitu ambavyo huonesha alama ya Utanzania ni ushabiki wa Simba na Yanga, namna tunavyocheza staili zetu kama vile kiduku, Takeu, Mduara, Mchiriku, mdundiko na, bia ya Kilimanjaro ambayo imetengenezewa kwa malighafi ya Tanzania.
Pia hata lugha zetu ambazo zinatumika mitaani ambazo hutufanya kuelewana kama kula bata, Piga tarumbeta, Mzuka, Chana Mic na mengineyo.
Msimamizi Mkuu wa promosheni hiyo kwa nyanda hiyo, Hafidh Abdallah akizungumzia kuhusu maendeleo ya promosheni hiyo kwa Nyanda za Juu Kusini, anasema anashukuru wakazi wa nyanda hizo kuipokea vizuri promosheni hiyo kwani kila kona watu wanaizungumzia.
Anasema ushiriki wa wakazi hao umekuwa mzuri kutokana na matangazo waliyoyafanya ya barabarani na hata kwenye vyombo vya habari, hivyo imesaidia kwa kiasi kikubwa promosheni hiyo kwenda vizuri.
"Kama ilivyo kauli mbiu yetu ya promosheni hii ya kuwataka Watanzania kutukuza vitu vyenye asili yao siku zote na ndio maana, wakazi wa Nyanda za Juu Kusini wamelitambua hilo na wanajitokeza kwa wingi," anasema Abdallah.
Anasema kadri wanavyotoka mkoa mmoja kwenda mwingine ndivyo ushiriki wa watu katika kuangalia promosheni yao inavyoongezeka na imesababisha hata unywaji wa bia ya Kilimanjaro Lager kuongezeka zaidi.
Alisema chombo cha mawasiliano katika kampeni hiyo ni stempu ya 100% Tz Flava ambayo imetengenezwa ili kumpa mteja raha lakini pia lazima iache ujumbe.
Anasema mpaka sasa mikoa ambayo tayari wameshaipitia ni Iringa, Ruvuma na Mbeya ambapo hivi karibuni wanatarajia kwenda Rukwa.
Nao Wapiga picha wa promosheni hiyo, Christ Shitindi na Diones Nyato ambao wamefanya ziara katika mikoa mbalimbali, wanazungumzia promosheni hiyo kwa kusema imefanya vizuri kwani jamii imejitokeza kwa wingi kila wanapokwenda.
Shitinda anasema mkoani Kagera promosheni hiyo imefanya vizuri kutokana na Kikundi cha Burudani cha Bombeso kukonga nyoyo za wakazi wengi kutokana na jinsi kinavyoelezea vitu vinavyomtambulisha Mtanzania.
"Kiukweli Promosheni ya 100% Tz flava imewaunganisha wakazi wengi wa Kagera kwani kila mtu sasa hivi anajivunia kujua ni vitu gani vinavyomtambulisha Mtanzania," anasema Shitindi na kuongeza;
"Ukikaa nao na ukiwaambia kupiga tarumbeta, wanajua ni kunywa bia au kula bata kwa maana ya kujirusha sehemu mbalimbali, hivyo ukiweza kutambua hayo ni dhahiri utakuwa umeielewa promosheni ya 100% tz Flava."
Anasema promosheni hiyo imewaunganisha watu wengi hata wale ambao walikuwa sio marafiki waliunganishwa kwa kushiriki katika mashindano mbalimbali ya kama kucheza muziki na kuimba.
Anasema promosheni hiyo hana shaka matumizi ya vitu vigeni vitapungua na Watanzania wataanza kuthamini vya kwao.
Naye Nyato ambaye amezunguka na bia hiyo katika mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro, anasema ni promosheni ambayo imefanya vizuri katika mikoa hiyo ambapo kwa kiasi kikubwa hawakupata shida kutokana na vitu vyote kujieleza.
Anasema promosheni hiyo ipo wazi kwamba inawaunganisha watanzania pamoja huku wakitambua vitu vinavyomtambulisha Mtanzania , kitu ambacho mkikutana nje ya nchi mnaweza kuzungumza lugha moja.
Anasema hakuna asiyeijua Simba au Yanga, kucheza kiduku, mduara, bongo flava au baadhi ya misemo kama kula bata, kupiga tarumbeta ni baadhi ya vitu ambazo Mtanzania anajivunia kuwa navyo.
Anasema akiwa Kilimanjaro walifanya promosheni katika Wilaya za Same, Moshi Vijijini, Mwanga, Rombo, Hai na Siha ambapo watu wa rika lote walijitokeza kushiriki promosheni hiyo ambayo imeacha gumzo mkoani humo.
"Tulikuwa tunawaauliza maswali mbalimbali kuhusu vitu vinavyowaunganisha na wengi hawatoki ndani ya vitu vinavyozungumzwa kila kukicha ambapo kama si shabiki wa Simba au Yanga, atapenda muziki wa taarabu au bongoflava," anasema Nyato.
Anasema Arusha walifanya promosheni hiyo Maji ya Chai na Manyara ni Merelani ambapo wakazi wengi wa humo wameielewa kwa haraka promosheni hiyo kupitia michezo na burudani.
Kampeni hiyo ya kuwaunganisha watanzania pamoja imepangwa kutumia sh. bilioni 2.3 za Kitanzania kwa kipindi cha miezi sita.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment