Na Mwandishi Wetu, Mwanza
MAJAJI wa mashindano ya kusaka vipaji wa Epiq Bongo Star Search (EBSS) 2012, jana wametoa somo la muziki kwa vijana waliojitokeza katika usaili kuwania nafasi ya kuwakilisha Mkoa wa Mwanza katika michuano hiyo ya kuimba.
Katika usaili huo uliofanywa na majaji, Salama Jabir, Master J na Ritha Paulsen ambao wamekuwa katika tasnia ya muziki kwa muda mrefu, wametumia muda mwingi kuwashauri vijana kuhusu mbinu za kufanikiwa katika muziki.
"Tunawaeleza kuhusu soko la muziki na aina ya nyimbo za kuimba ili wafanikiwe, hiyo ni sehemu ya kazi yetu, lakini pia vijana wengine tumewashauri kujiunga na fani nyingine ambazo tumeona wana vipaji, kama uigizaji au uanamitindo," alisema Jaji Mkuu, Ritha.
Vijana wengi waliojitokeza waliwapongeza majaji kwa elimu hiyo ya muziki wakisema wamefurahia ushauri huo na utawasaidia katika kujiendeleza kisanaa.
‘Unajua hawa majaji wamefanya hili kazi kwa miaka mingi hivyo ni wazoefu na wakikwambia huwezi, jaribu kitu kingine unapaswa kuelewa," alisema mmoja wa washiriki, Baraka Juma.
Akizungumzia Mkoa wa Mwanza, Ofsa Biashara wa Zantel, Sajid Khan alisema mashindano ya mwaka huu ni zaidi ya kutafuta vipaji.
"Kama unavyoona tuna shughuli za utoaji damu zinaendelea hapa, ambapo Mwanza zaidi ya mikoa yote naona hamasa imekuwa kubwa sana," alisema Khan.
Mshindi wa mwaka huu katika mashindano hayo atajinyakulia sh. milioni 50 na mkataba wa kurekodi kutoka Zantel
No comments:
Post a Comment