06 July 2012

EBSS sasa kuvamia Arusha kesho



Na Mwandishi Wetu, Arusha

BAADA ya kumaliza ziara ya kusaka vipaji katika mikoa mbalimbali, Epiq Bongo Star Search (EBSS) kesho imejipanga kuvamia jijini Arusha kutafuta vipaji vya mkoa huo.

Jiji la Arusha linatarajia kutoa ushindani mkubwa katika kutafuta vijana, katika kazi ya siku mbili itakayofanyika katika Ukumbi wa Triple A, huku shauku ikiwa kubwa ni vijana gani watafanikiwa kuuwakilisha mkoa huo kati ya maelfu watakaojitokeza.


Jaji Mkuu wa EBSS, Ritha Poulsen alisema ikiwa imebakiza majiji manne ambayo ni Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Tanga na Mbeya hamasa imekuwa kubwa zaidi.

"Majiji yote yaliyobaki yanafahamika kwa wanamuziki wengi maarufu wanaotokea sehemu hizo, kwa mfano Arusha, imetoa wanamuziki wengi nyota na hivyo kama Epiq Bongo Star Search tunatarajia kupata vijana wenye vipaji wengi zaidi kutokea hapo," alisema Ritha.

Alisema katika mikoa ya Lindi, Dodoma na Zanzibar wameshaona vipaji vingi na vikubwa hali inayompa imani kuwa katika maeneo wanayokwenda hali itakuwa nzuri zaidi.

“Mikoa ambayo tumeshaitembelea hali imekuwa nzuri tumeona vipaji vya ukweli na moto kweli kweli kama Epiq Moto, sasa majaji tumejipanga kuhakikisha kuwa huku tuendako tutakuwa na wakati mgumu wa kuchagua vijana kwa kuwa vipaji ndiyo vitakuwa vingi zaidi,” alisema.

Akizungumzia mashindano hayo, Mkuu wa Mawasiliano wa Zantel ambao ndiyo wadhamini wakuu, Awaichi Mawalla aliesema anaamini mashindano hayo yatakuwa ya kipekee mwaka huu, kutokana na udhamini walioutoa na vitu vingi vipya ambavyo Zantel, wamejipanga kuwapatia mashabiki wa EBSS.

"Tunataka mashindano haya yawe na viwango vya kimataifa na ndiyo maana tumeongeza vitu vingi vipya, ikiwepo zawadi ya sh. milioni 50 ili kuongeza ushindani," alisema Awaichi.


No comments:

Post a Comment