11 July 2012

Dkt. Mkopi aburutwa kortini Kisutu *Ashtakiwa kwa kukaidi amri ya kuzima mgomo *Mawakili wa Serikali wamng'ang'ania, wakwama


Rehema Mohamed na Stella Aron

RAIS wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dkt. Namala Mkopi, jana alipandishwa kizimbani katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, akikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kukiuka amri ya kusitisha mgomo wa madaktari iliyotolewa na Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi.

Dkt. Mkopi ambaye anatetewa na jopo la mawakili wanne ambao ni   Dkt. Lumegeneza Nshala, Dkt. Mauridi Kondo, Dkt. Gaston Kenedy wakiongozwa na  Bw. Isaya Matambo, alipandishwa kizimbani mbele ya Hakimu, Bw. Faisal Kahamba na kusomewa mashtaka yanayomkabili.

Wakili Mwandamizi wa Serikali, Bw.Tumani Kweka, akishirikiana na Bw. Ladslaus Komanya, alidai katika kosa la kwanza, mshtakiwa huyo anakabiliwa na shtaka la kukiuka amri ya Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi aliyotolewa kwa tarehe tofauti kati ya Juni 26 na 28 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Alidai kuwa, mshtakiwa akiwa Rais wa MAT, alikiuka amri ambayo ilitolewa Juni 26 mwaka huu iliyomtaka atoe tangazo kwa wajumbe wa chama hicho kupitia vyombo vya habari la kutoshiriki mgomo.

Mshtakiwa alitakiwa kutoa tangazo hilo kama amri ya awali ilivyotolewa na mahakama hiyo Juni 22 mwaka huu.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa Juni 27 mwaka huu, jijini Dar es Salaam, mshtakiwa aliwashawishi wajumbe wa MAT kushiriki mgomo kinyume na amri ya Mahakama Kuu, Kitengo cha Kazi iliyotolewa Juni 22 mwaka huu.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, mshitakiwa alikana kutenda makosa yote mawili ambapo upande wa mashtaka ulidai kuwa, upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika.

Hata hivyo, Dkt. Mkopi aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ambayo ni kuwa wadhamni wawili wanaofanya kazi katika taasisi za Serikali ambao wamesaini hati ya dhamana ya sh. 500,000 kila mmoja.

Awali upande wa mashtaka ulipinga masharti ya dhamana yaliyotolewa Hakimu Bw. Kahamba anayesikiliza kesi hiyo wakitaka mahakama izingatie kifungu namba 148 kifungu kidogo cha 6 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai sura ya 20.

Kifungu hicho kinamtaka mshtakiwa kuwasilisha mahakamani hati yake ya kusafiria na kutotoka nje ya Dar es Salaam bila ya kibali maalumu cha mahakama.

Pia upande wa mashtaka ulimpinga mdhamini mmoja kati ya hao kwa madai ya kufanyakazi katika taasisi moja na mshtakiwa hivyo kunaweza kuleta dosari na ukizingatia shauri hilo linahusu mgomo.

Hakimu Bw. Kahamba, aliueleza upande wa mashtaka kuwa anachojua yeye kifungu hicho kimeshafutwa na Mahakama Kuu.

Aliongeza kuwa, kifungu hicho kinaipa uhuru mahakama kutoa masharti mengine yanayofaa hivyo masharti aliyotoa yanafaa na kama kuna upande ambao haujaridhika una haki ya kukata rufaa.

Kuhusu mdhamini kufanya kazi taasisi moja na mshtakiwa, Hakimu Kahamba alisema hakizuii dhamana.

“Hatufanyi hivyo kukomoana, bali haki inatendeka, kama nilivyosema kama kuna upande haujaridhika una haki ya kukata rufaa Mahakama Kuu, mimi naona wadhamni wametimiza vigezo,” alisema.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 6 mwaka huu, itakapotajwa tena. Wakati huo huo, baadhi ya madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili na Taasisi ya Tiba na Mifupa (MOI), walishangazwa na hatua ya kukamatwa kwa kiongozi huyo na kudai kitendo hicho kitasababisha kudhoofisha ari ya utendaji kazi iliyokuwa imeanza kuimarika.

Wakizungumza na Majira, walidai ni bora Serikali ingemaliza kutatua suala la madaktari ili kuendelea na masuala mengine kwa kutafuta suluhu kwenye vyombo vya sheria.

Hata hivyo, huduma katika Hospitali Taifa Muhimbili pamoja na MOI, jana ziliimarika zaidi.

Ofisa Habari wa taasisi hiyo, Bw. Almasi Jumaa, alisema idadi ya wagonjwa waliotibiwa hadi jana mchana ilikuwa 177 tofauti na siku za nyuma.

Naye Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Bw.Aminiel Aligaeshi, alisema vitengo vyote jana vilianza kutoa huduma huku idadi ya wagonjwa ikiongezeka zaidi.

“Hivi sasa wagojwa wanaweza kuja na kupata huduma, vitengo vyote vinafanyakazi tofauti na kipindi cha nyuma,” alisema.

4 comments:

  1. So madaktari hamna umoja tena. Mmesambaratishwa na mkasambaaa.

    ReplyDelete
  2. JE KUNA UMOJA KATIKA KILA MMOJA DHAMIRI YAKE INAMHUKUMU TOFAUTI ANAVYOSABABISHA VIFO VYA WATADU IDADI GANI MIZIMU YA MAREHEMU ITAWASUMBUA SANA WANAWEZA KUSHINDA DUNIANI SI KUZIMU AJIRA ZINGINE UCHURO TUPU

    ReplyDelete
  3. wajinga ninyi, hamjua matatizo ya madaktari na mnatetea ujinga.Raisi wenu anavyotumia pesa za nchi kwa anasa wakati madawa hayapo mahospitalini mnaona poa sio??

    wabunge wanavyojiongezea posho wanavyotaka mnaona poa sio?

    jifunzeni kufikiri .

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hivi wauaji hasa ni wapi? Wanaoendekeza anasa kwa jasho la Watanzania bila kujali wanaokufa kwa kukosa vifaa tiba kama X-ray machines, t-scanners n.k. madawa, wodi, vitanda au wale wanaogoma na kusababisha vifo ili kuwaamsha wazembe serikalini. Angalia bajeti ya chai, safari za viongozi nje, matibabu ya viongozi, posho za vikao n.k na bajeti ya huduma za afya ndipo utagundua nani anayestahili kupelekwa mahakamani

      Delete