BAADA ya kutamba kwa muda mrefu katika muziki wa kizazi kipya nchini, msanii nyota wa muziki huo, Naseeb Abdul ‘Diamond’ amesema anafikiria kujitosa katika muziki wa taarab.
Diamond alisema mjini Dar es Salaam wiki hii kuwa, amefikia uamuzi huo kutokana na kuvutiwa na muziki huo wa taarab.
Mshindi huyo wa tuzo mbalimbali za muziki za Kilimanjaro amesema, anajua uamuzi wake huo utawashangaza mashabiki wengi, lakini ni jambo la kawaida kwa msanii.
Diamond alisema hadi sasa anaamini hana mpinzani katika muziki wa kizazi kipya na hakuna msanii anayeweza kufikia kiwango chake hapa nchini.
“Najua watu watanishangaa na kuniona mtu wa ajabu, lakini nimefanya hivyo kwa sababu sina mpinzani katika muziki wa kizazi kipya,”alisema.
Diamond alisema ameamua kupiga miondoko tofauti ya muziki kutokana na kipaji alichonacho katika fani hiyo, ambayo imempatia umaarufu mkubwa.
Kutokana na kipaji chake hicho, Diamond alisema hakuna kitu anachoshindwa kukifanya katika muziki.
“Bado sijaanza rasmi kupiga muziki wa taarab, ninachokifanya kwa sasa ni kufanya tathmini ya soko lake ili kuona kama unaweza kuniletea mafanikio kama ilivyo kwa muziki wa bongo fleva.
“Naweza kufanya kila aina ya muziki kwa sababu nina kipaji cha kuimba nyimbo aina zote, hivyo endapo nitafikia muafaka, naweza kufanya kitu hicho ingawa mashabiki wangu watashtuka sana,” alisema.
Diamond alikiri kuwa, muziki wa kizazi kipya umemfanya ajulikane sehemu nyingi duniani, ikiwa ni pamoja na kupata manufaa mbalimbali kimaisha kwa kuishi kwenye nyumba nzuri na kumiliki magari ya kifahari.
No comments:
Post a Comment